Thursday, June 14, 2012

Sijakichukia chama




CHAMANI nimezaliwa, siwezi chukia chama,
Baba na mama radhia, ni wa mwanzo waokuwa,
Leo wameshajifia, mwenyewe nimebakia,
Sijakichukia chama, ni uchama nakataa !

Na shule nilipokuwa, yusiligi nilikuwa,
Na chipukizi tambua, kiongozi nilikuwa,
Moshi tukisimamia, na Frismila pia,
Sijakichukia chama, ni uchama nakataa !

Ila yanayotokea, kichefu yananitia,
Na mbali nimeamua, yote kuyaangalia,
Karibu sintosogea, udhu wangu kutengua,
Sijakichukia chama, ni uchama nakataa !

Kingine sintoingia, bado ninawazimia,
Mapinduzi nangojea, kweli yatakayokuwa,
Ujanja ukiishia, mapenzi nitarudia,
Sijakichukia chama, ni uchama nakataa !

Hodi mnaonipigia,  mlango sintofungua,
Majina ninawajua, sijazijua tabia,
Maradhi mliy9kuwa, kutoniambukizia,
Sijakichukia chama, ni uchama nakataa !

Yapo mnayoyajua, mengi yasiyotufaa,
Haya mkzungumzia, na mengi mtagundua,
Mtu usipojijua, vipi gamba utavua,
Sijakichukia chama, ni uchama nakataa !

Historia yaanzia, Baba  ' lipojiondoa,
Na aliyefuatia, sisi sote twamjua,
Mizizi hakuitia, juujuu alikuwa,
Sijakichukia chama, ni uchama nakataa !

Na aliyemfatia, kila kitu kaachia,
Na leo wetu ukiwa, hapo kwake yaanzia,
Kusema ninakataa, ndivyo  'livyoandikiwa,
Sijakichukia chama, ni uchama nakataa !

Sasa chini wabakia, waacha juu bakia,
Heshima wakaitwaa, taifa kusimamia,
Hii ni kubwa balaa, na mwalimu alijua,
Sijakichukia chama, ni uchama nakataa !

Wazee mnaojua, waambieni jamaa,
Uchama kuuachia, utaifa ukawajaa,
Wote ni Watanzania, nchi hii tuna hawa,
Sijakichukia chama, ni uchama nakataa !

Ubaguzi nahofia, kwetu hapa Tanzania,
Kusini tulikataa, kwanini kuuridhia ?
Ni aibu itakuwa, ikitujua dunia,
Sijakichukia chama, ni uchama nakataa !

Ni ukabila mpya, nchini tunauzua,
Sisi  kujipendelea, wengine tukawaonea,
Amgalieni Syria, leo yanayotokea.
Sijakichukia chama, ni uchama nakataa !

No comments: