Tuesday, June 12, 2012

Kila awaye mtusi



KWA mropoka matusi, hivi kweli anajua,
Kwa kila wake utusi, neno linamrejea,
Ama hiki kinamasi, wachache wanaojua,
Kila awaye mtusi, hujitukana wenyewe !

Kiumbe nje ya nafsi, roho moja tunakuwa,
Ukilitia kamasi, nalo lako linakuwa,
Na ukikipaka kinyesi, nawe kitakuenea,
Kila awaye mtusi, hujitukana wenyewe !

Ukiwa ni muflisi, waifilisi dunia,
Mtu kama wasiwasi, kiumbe ameumbiwa,
Nafsi ni ubinafsi, na utu ni majaliwa,
Kila awaye mtusi, hujitukana wenyewe !

Nafsi kama chunusi, kila mtu huchukua,
Si hodari kwa ususi, yake hayachi fumua,
Haijawa ni libasi, mwenyewe tu aijua,
Kila awaye mtusi, hujitukana wenyewe !

Za balaa na nuksi, ndivyo zinavyozaliwa,
Wengi wetu ni mijusi, na vikenge twazaliwa,
Hatuitoi nafasi, wengine wakajaliwa,
Kila awaye mtusi, hujitukana wenyewe !

No comments: