Thursday, June 14, 2012

Chama sasa ni mradi

USANII waingia, vyama vinanunuliwa,
Dau kubwa wanatoa, fisadi kuviingia,
Na nafasi kuzitwaa, ukubwa wakajaliwa,
Chama sasa ni mradi, tena wa watu wachache !

Bahasha mnazopewa, ruzuku yenu yaliwa,
Mapya wanafukua, ya zamani kufukia,
Na wajinga wanaliwa, bilal ya kujitambua,
Chama sasa ni mradi, tena wa watu wachache !

Mafuta mnayotoa, wenyewe mwakaangiwa,
Hii ndiyo Tanzania, na majuha ndio hawa,
Kila ukifikiria, hautaiona ndia,
Chama sasa ni mradi, tena wa watu wachache !

Miradi wafikiria, hewani ikaishia,
Hadithi imebakia, vichanga wanavyoua,
Wakabaki tegemea, haamu vilivyokuwa,
Chama sasa ni mradi, tena wa watu wachache !

Biashara twasomea, wenzetu watukataa,
Kujua wanajitia, na haweshi kufulia,
Hadimu wamezoea, ridhaa wanaotoa,
Chama sasa ni mradi, tena wa watu wachache !

Hawataki walokua, wanakikinga kifua,
Na yao  wakakataa, kufuja yanapokuwa,
Miradi kutojifia, ikazidi kuchanua,
Chama sasa ni mradi, tena wa watu wachache !

Wanataka wenye njaa, kila kitu kwitikia,
Hata na yasiyofaa, wakaja kuyajutia,
Hilo nami nakataa, siwezi kuwasaidia,
Chama sasa ni mradi, tena wa watu wachache !

Kofia ningelipewa, mbona ningewanyanyua,
Kwani mimi si adawa, chama sijakikimbia,
Ila mwafanya nazaa, mtakayokujajutia,
Chama sasa ni mradi, tena wa watu wachache !

Siasa ni majaliwa, kwa wengine ni vipawa,
Na wapo wasiokuwa, ila mengine wajua,
Akili wanaokua, hili wapaswa kujua,
Chama sasa ni mradi, tena wa watu wachache !

No comments: