Tuesday, June 12, 2012

I S I Y O S I R I B A R U A



Japo ninayo mafua, na tena ninakohoa,
Hadhari ninaitia, msemalo kulijua,
NInawafuatilia, ndugu zangu waheshimiwa,
Kazi hii nimetumwa, siwezi kuichezea !

ISIYO SIRI BARUA, kaumu naiachia,
Kusinzia twakataa, lazima maji kumwaiya,
Macho mkaangazia, na sauti kusikia,
Kazi hii nimetumwa, siwezi kuichezea !

Ujumbe nimetumiwa, hili kulishindilia,
Mstari kuutia, mweusi uliokuwa,
Macho yawaangazia, ujinga kuukataa,
Kazi hii nimetumwa, siwezi kuichezea !

Kukubali msojua, itakuwa ni hatia,
Raia njaa walia, na nafuu wangojea,
Gharama zikipungua, afueni watajua,
Kazi hii nimetumwa, siwezi kuichezea !

Kusoma mnatakiwa, uvivu kuukataa,
Kila kitu kuchimbua, hatari kuziondoa,
Na bajeti kuielewa, isiwe kwenu kulewa,
Kazi hii nimetumwa, siwezi kuichezea !

Punguzeni kutembea, kuiganga yetu njaa,
Na muda mfupi ukawa, yenu kuzungumzia,
Wengi twalala na njaa, sakafu 'kikumbatia,
Kazi hii nimetumwa, siwezi kuichezea !

Nchi hii Tanzania, hamsini inshakua,
Miaka ya kukomaa, makubwa kujifanzia,
Utotoni twabakia, bila sababu kujua,
Kazi hii nimetumwa, siwezi kuichezea !

Katika hii dunia, nani atasaidia,
Wazungu wanaugua, njaa imewavamia,
Reli watawajengea, au  hii ni sanaa ?
Kazi hii nimetumwa, siwezi kuichezea !

Vigelegele potea, na kuishe kuzomea,
Mwatakiwa kuongea, ya juu kufikiria,
Kwanini twatambaa, na wala si kupaa,
Kazi hii nimetumwa, siwezi kuichezea !

Ulizeni injinia, uwezo hawajajaliwa,
Hawawezi tuundia, matrekta yakafaa,
Teni pasenti yaua, mabovu twaagizia?
Kazi hii nimetumwa, siwezi kuichezea !

Kaulizeni injinia, barabara kuenea,
Kama kwao ruia, kazi wataikimbia,
Au nyanya tushakua, kudekeza twakolea?
Kazi hii nimetumwa, siwezi kuichezea !

Kaulizeni injinia, kama reli nayo pia,
Kujenga itawaumbua, hawawezi kuchimbua,
Hata mkiwapatia, vifaa vinavyotakiwa,
Kazi hii nimetumwa, siwezi kuichezea !

Kaulizeni injinia, kwanini wanafulia,
Hata kompyuta pia, lazima kuagizia,
Au tumekwishalemaa, magongo twatembelea?
Kazi hii nimetumwa, siwezi kuichezea !

Au tumekwishalemaa, magongo twatembelea?
Sindano jamani pia, nje eti twanunua,
Hata pasi naambiwa, kigeni zinatumia?
Kazi hii nimetumwa, siwezi kuichezea !

Kaulizeni injinia, kama waweza pangua,
Gari  wakatambua, kitu gani chatakiwa,
Kisha wakajiungia, gari kuwa kwa spea,
Kazi hii nimetumwa, siwezi kuichezea !

Ninawasikitikia, vijana kusahauliwa,
HIzi kazi zingekuwa, wenyewe twajifanyia,
Huku wanasaidiwa, na Wazungu ulua,
Kazi hii nimetumwa, siwezi kuichezea !

Amkeni wajamaa, kazi tuache kimbia,
Mawaziri mwatakiwa, na wabunge nao pia,
Kwenye ujenzi kwingia, nchi ikaendelea,
Kazi hii nimetumwa, siwezi kuichezea !

Hatuwezi mtegemea, mjomba hatukujaliwa,
Kila kitu nawambia, lazima kujifanzia,
Na hapo ukubwa 'kawa, sasa mwajiringia,
Kazi hii nimetumwa, siwezi kuichezea !

Nini mnachoringia, hali kwenu kuna njaa ?
Na nchi zenu majaa, takataka mwatupiwa,
Kiooni angalia, aibu utaijua,
Kazi hii nimetumwa, siwezi kuichezea !

Bunge hili natambua, kuna vichwa vya kufaa,
Budi kuchangamkia, kauli ni maridhawa,
Ila asiyetambua, hduhani adhihakiwa,
Kazi hii nimetumwa, siwezi kuichezea !

Uzalendo twaujua, sio sifa na nazaa,
Uzalendo kulilia, nchi  ukaiagua,
Maradhi ukayatoa, nchi ikaendelea,
Kazi hii nimetumwa, siwezi kuichezea !

Uzalendo naujua, si ndani kukomalia,
Nje yanayotokea, huwezi hata kujua,
Maisha wafurahia, hali nchi inalia ?
Kazi hii nimetumwa, siwezi kuichezea !

Uzalendo kuwazia, makubwa kujifanzia,
Tena wenyewe mkawa, sio kwa kutegemea,
Kujinyima kuamua, mpate kufaikiwa,
Kazi hii nimetumwa, siwezi kuichezea !

Miradi inatakiwa, ya kwetu ya asilia,
Shida zetu twazijua, hizo ndio za kuondoa,
Vipi tunajitania, kudhani tume'ndelea?
Kazi hii nimetumwa, siwezi kuichezea !

Mimi bado mjamaa, ubepari kwangu baa,
Kwenye nchi  ilovia, ufisadi inakuwa,
Majukumu wasoujua, ndio vyeo wanapewa?
Kazi hii nimetumwa, siwezi kuichezea !

Na elimu yatakiwa, matatizo kutatua,
Hela zetu zapotea, kufunza yasiyokuwa,
Tisini asilimia, haiji ikatumiwa,
Kazi hii nimetumwa, siwezi kuichezea !

Mipango kuifumua, malengo isiyokuwa,
Ya nchi kuendelea, na wala si kutumia,
Na ajira kuzizua, mapato kujipatia,
Kazi hii nimetumwa, siwezi kuichezea !

Heri ninawatakia, wetu watunga sheria,
Akili kwenda zinoa, sasa waje na mapya,
Tanzania kunyanyua, nafuu tukaijua,
Kazi hii nimetumwa, siwezi kuichezea !




No comments: