Tuesday, June 12, 2012

Mmarikani mweusi

Waliosahau akili, ndiyo wanayojaliwa,
Huizidisha akili, hata uchi  kutembea,
Wakajiona aghali, kumbe si kitu wakawa,
Mmarikani mweusi, yu kama nyani wamwiga ?

Mbona nauona muhali, kijana kujivalia,
Makalio kitu ghali, urahisi kuyatia,
Moto yakiunakili, wewe utaweza kaa ?
Mmarikani mweusi, yu kama nyani wamwiga ?

Umbo lako la jamali, na mtumwa haujawa,
Kiumbe wewe halali, haramu unajitia,
Umekuwa ni anzali, lako usilolijua?
Mmarikani mweusi, yu kama nyani wamwiga ?

Hao sio watu ghali, urahisi wajitia,
Zimedhurika akili, kwa kuwa wanaonewa,
Wakafanziwa rijali, wenyewe kujichukia,
Mmarikani mweusi, yu kama nyani wamwiga ?

Ndugu zao wanawali, mikononi watingia,
Kufurahisha fahali, wa kizungu walokuwa,
Wakajiona dhalili, uwezo kutojaliwa,
Mmarikani mweusi, yu kama nyani wamwiga ?

Kila wanachonakili, kina ujumbe watoa,
Ndugu yangu bwana Ally,  kitu gani watwambia ?
Na nani kasema mali, kutangaza ndiyo njia ?
Mmarikani mweusi, yu kama nyani wamwiga ?

Hawa watu wa shubili, asali yawachefua,
Wamekosa maadili, kwayo hawakuzaliwa,
Ni jamii ya ajali, waliyokwishaandikiwa,
Mmarikani mweusi, yu kama nyani wamwiga ?

Usiwaige dhalili, udhani juu wakwea,
Utajitia kabali, na miguu kuugua,
Ukajiona si hali, na ndoto kukupotea,
Mmarikani mweusi, yu kama nyani wamwiga ?

Ninamuomba Jalali, wanangu wakajijua,
Tabia wasibadili, kwa Afu kumhofia,
Yangu wakayakubali,  ndiyo ifaayo njia,
Mmarikani mweusi, yu kama nyani wamwiga ?

No comments: