Tuesday, June 12, 2012

Nikubalishe mengine



Huenda nikakubali, kiasi yaliyokuwa,
Ambayo ni makubuli, fikra ukitumia,
Lakini haliwi hili, la ahadi kuhadaa,
Nikubalishe mengine, ila sio la kuzua !

Utafanza kulhali, hili bado nakataa,
Kwangu mimi ni muhali, historia naijua,
Kumwabudu mwanamwali, hilo kwangu halijawa,
Nikubalishe mengine, ila sio la kuzua !

Kusema kuna wawili, hadi kiama nakataa,
Naijua bilkuli, kauli ameshatoa,
Na laana sio ghali, na ameshawatupia,
Nikubalishe mengine, ila sio la kuzua !

Hawaoni mushkeli, macho hawajafunguliwa,
Na uzungu wa itikeli, kcihwani umeshaingia,
Ni dhoofu bin hali, vigumu kujitambua,
Nikubalishe mengine, ila sio la kuzua !

Wamekazania mali, upepo inayofagia,
Na yahudi kukubali, kiongozi wao kuwa,
Kwangu mimi ni ajali, tena iokuwa mbaya,
Nikubalishe mengine, ila sio la kuzua !

Waukataa ukweli, japo wanajionea,
Wajidhania kamili, kumbe sana wapungua,
Ibilisi hana hali, yake wameshachukua,
Nikubalishe mengine, ila sio la kuzua !

Utadhani ni anzali, hawana wanalojua,
Na wasomi wa amali, ndani kwao wamejaa,
Na kila mwenye akili, hugeuzwa eti juha,
Nikubalishe mengine, ila sio la kuzua !

Tunaziona dalili, ndani kinachotokea,
Wajanja wanasaili, ya kwao kupalilia,
Waishushe idhiliali, sio mbali nawambia,
Nikubalishe mengine, ila sio la kuzua !

Zitamwagika amali, mashuhuri walokuwa,
Ikaangaza kandili, juu itakayotokea,
Na mjumbe sijadili, sijui itavyokuwa,
Nikubalishe mengine, ila sio la kuzua !


No comments: