Tuesday, June 12, 2012

Wakowapi watu wema ?

Watu wema nauliza, wapi wamejikalia?
Hatuna ila ni viza, mayai yaliyokuwa,
Kuangua miujiza, hili nanyi mnajua,
Wako wapi watu wema, watukurubishe na Mola ?

Tumeshajipatiliza, maridhia'toridhia,
Machoye kayaangaza, watu wanavyoumia,
Kusilimu, kubatiza, nini kitasaidia ?
Wako wapi watu wema, watukurubishe na Mola ?

Shiriki inatuponza, chuki pia na ubaya,
Na wengine kuwaiza, imani zao kuvia,
Yangu mkayakataza, yenu mkaangalia,
Wako wapi watu wema, watukurubishe na Mola ?

Itokee miujiza, ya sindano na ngamia,
Kwa mnaojipendekza, mkadhani mwanifaa,
Moto mnauchokoza, nilosema kukataa,
Wako wapi watu wema, watukurubishe na Mola ?

Yangu mmeshayazoza, hata nami nachukia,
Nyoyo mngezikataza, ya uongo kuyazua,
Wengine kuwaumiza, furaha kwenu ikawa,
Wako wapi watu wema, watukurubishe na Mola ?

Mwafaa kujiuguza, kwa ninayowaandalia,
Ila kama mtaweza, tawba kuililia,
Yangu mkatanguliza, yenu kisha kufwatia,
Wako wapi watu wema, watukurubishe na Mola ?

Mimi si mtu wa giza, nuru ndio yangu njia,
Hakuna nisiloweza, ila napenda wa'chia,
Yangu mkatengeneza, safi njia yenu kuwa,
Wako wapi watu wema, watukurubishe na Mola ?

Mimi ni bwana wa kukwaza, kadhalika nakwamua,
Ni bwana wa kutengeza, pia nawaharibia,
Wote wanaotangaza, kitali kunizulia,
Wako wapi watu wema, watukurubishe na Mola ?

Mimi ndiye miujiza, na ibara zashangaa,
Huongeza, hupunguza, na hutoa na hutwaa,
Baraka nikitangaza, hakuna wa kuwafikia,
Wako wapi watu wema, watukurubishe na Mola ?

No comments: