Saturday, June 2, 2012

Viongozi si wananchi



WAIFILISI dunia, tena bila ya huruma,
Kikubwa wamezoea, hali wnegine wanyimwa,
Sasa njaa imekua, yabidi kulitazama,
Viongozi si wananchi, waifilisi dunia !

Chakula kimepungua, katika dunia nzima
Milo mitatu kutia, watu watakutazama,
Hudhaniwa roho mbaya, tena huna taadhima,
Viongozi si wananchi, waifilisi dunia !

Shilingi imefubaa, kazidiwa wake mama,
Dola ameshafulia, kila mtu anasema,
Siku hazijapitia, yaweza kuwa marhuma,
Viongozi si wananchi, waifilisi dunia !

Mchina kachachamaa, anaitaka heshima,
Ataka kuinunua, dunia ikimtazama,
Na saluti kuitoa, huyu ni yule wa zama,
Viongozi si wananchi, waifilisi dunia !

Dunia inatakiwa, upya kujitazama,
Zama zimeishilia, mengine siyo lazima,
Matatizo ya dunia, ni upande yaegema,
Viongozi si wananchi, waifilisi dunia !

Ndani unapoanzia, wote bado twaroroma,
Ukweli hatujajua, twazitoa tu kalima,
Kiini kimechimbiwa, nasi hatuna tuhuma,
Viongozi si wananchi, waifilisi dunia !

Wengi walijigawia, kwingine walikofuma,
Nyara wakajitwalia, kadri walivyozama,
Hakuna aliyesama, nani alijitambua,
Viongozi si wananchi, waifilisi dunia !

Leo wana wamekua, waona dunia nzima
Yao wanayatetea, kidete wamesimama,
Wataka kujichumia, ama Ulaya kuzama,
Viongozi si wananchi, waifilisi dunia !

Hawahofu kujifia, kuliko hapa kukwama,
Melni watachupia, na kwenye ndege kutoma,
Hata wakining'inia, hiyo ni bora salama,
Viongozi si wananchi, waifilisi dunia !

Zama zilizoishia, nchi zilikuwa nyuma,
Nyingine kutawaliwa, kama shamba kuazima,
Wapi leo utapewa, bure bure kulilima ?
Viongozi si wananchi, waifilisi dunia !

Mahala pa kuanzia, zaidi wanaochuma,
Kingi wakakiachia, wakaiondoa nakama,
Hili likikataliwa, dunia itarindima,
Viongozi si wananchi, waifilisi dunia !

Itarindima dunia, kwa balaa na nakama,
Watoto kujilipua, shilingi ukiwanyima,
Na ndoa zitajifia, ikabakia zahama,
Viongozi si wananchi, waifilisi dunia !

Kazi zikishapotea, akili zitawatuma,
Mambo kujifanyia, ya Gomorrah na Sodoma,
Ruhusa ameshatoa, mstahiki Obama,
Viongozi si wananchi, waifilisi dunia !

Wengine wanafatia, hawajui ni kiyama,
Wao wakifurahia, ushidi kuutazama,
Kumbe  ni kutojijua, dunia yetu yazama,
Viongozi si wananchi, waifilisi dunia !


No comments: