Tuesday, June 12, 2012

Hivi sasa wanachama

KAMA hili la hakika, inafaa kutazama,
Naambiwa imefika, zamu yao maamuma,
Wasiopo kuyashika, ya wengine kutazama,
Hata teja na vibaka, hivi sasa wanachama !

Uhakiki wapituka, zikazagaa tuhuma,
Wahesabika vibaka, hivi sasa wanachma,
Msajili hajataka, mmoja'moja kutazama,
Hata teja na vibaka, hivi sasa wanachama !

Hatunao uhakika, ya kusuka na kufuma,
Hivi nchi watashika, watu wanaororoma,
Na matusi kutapika, kama hii si nakama ?
Hata teja na vibaka, hivi sasa wanachama !

Chama kikastahika, wasafi budi kugema,
Hali isijechafuka, ukakuta unazama,
Magenge yaje kuzuka, ya rabsha na zahama,
Hata teja na vibaka, hivi sasa wanachama !

Budi kustaarabika, muungwana mwanachma,
Heshima akaiweka, mtu anapomtazama,
Akajua kwa hakika, hawa wetu wenye mema,
Hata teja na vibaka, hivi sasa wanachama !

No comments: