Tuesday, June 12, 2012

Chombo hiki kimeundwa

Kimeundwa chombo hiki, kiitwacho Mwafrika,
Kwa hadhari na Maliki, kiwe kitu cha hakika,
Na dunia kumiliki, siku yao ikifika,
Chombo hiki kimeundwa, kiitwacho Mwafrika !

Kaifanza hii kazi, mpaka akaridhika,
Akazishona kwa nyuzi, roho za kuaminika,
Na akazipanga enzi, yao yatavyofanzika,
Chombo hiki kimeundwa, kiitwacho Mwafrika !

Subira kawajalia, wavumiia mashaka,
Huku wanamrudia, kutafuta la hakika,
Na mida ikiingia, kutokuwa na wahaka,
Chombo hiki kimeundwa, kiitwacho Mwafrika !

Mitihani kaitia, isiyokuelezeka,
Hali anaitambua, siyo ya kudhindikika,
Abdi akawaachia, malaika kuandika,
Chombo hiki kimeundwa, kiitwacho Mwafrika !

Malaika walijua, naye wanafurahika,
Mbora huyu watambua, dunia atayeshika,
Na tukio walijua, ila si siku kufanzika,
Chombo hiki kimeundwa, kiitwacho Mwafrika !

Ajua wataachiwa, muda ukimalizika,
Imani zitapotakia, si majengo kwa hakika,
Na roho zitapotambua, lipi ndio la hakika,
Chombo hiki kimeundwa, kiitwacho Mwafrika !

Hili ukisimuliwa, ndugu yangu waokoka,
Kama utalisikia, na usiwe na haraka,
Mmoja wao ukawa, watu wenye muafaka,
Chombo hiki kimeundwa, kiitwacho Mwafrika !

Shairi namalizia, kwa dua kuitamka,
Shukrani kuitoa, kwa hii yetu baraka,
Tupushiwe balaa, siku hiyo ikifika,
Chombo hiki kimeundwa, kiitwacho Mwafrika !

No comments: