Tuesday, June 12, 2012

Ulozi wa mkoloni



Hatumtii machoni, lakini wake wamfaa,
Kawaachia  medani, vyake wazidi kulea,
Haunao yumkini, yake anajivunia,
Ulozi wa mkoloni, atubeba mgongoni:
Kamba akiziachia,
Lazima kuendelea !

Angalia hamsini, wengi wamezainiwa,
Wamejitia thamani, katu wasiyofikia,
Na kuona ahueni, pale pa kusikitikia,
Ulozi wa mkoloni, atubeba mgongoni:
Kamba akiziachia,
Lazima kuendelea !

Wameiivaa miwani, ya jua iliyokuwa,
Wadhania ya nyumbani, ndiyo pia ya mtaa,
Wasahau vijijini, walivyowashindilia,
Ulozi wa mkoloni, atubeba mgongoni:
Kamba akiziachia,
Lazima kuendelea !

Maendeleo wahini, vijiji vinadumaa,
Tokea enzi za jamani, hujuma na ujamaa,
Walipoletwa njiani, kusiko nayo mbolea,
Ulozi wa mkoloni, atubeba mgongoni:
Kamba akiziachia,
Lazima kuendelea !

Au kutupwa porini, jangwnani kulikokuwa,
Na wengine vichakani, kitu pasipojaliwa,
Wasifanziwe hisani, wakabaki wanalia,
Ulozi wa mkoloni, atubeba mgongoni:
Kamba akiziachia,
Lazima kuendelea !

Ilipokwama mizani, ukawajaa ukimya,
Wapiga abautani, wasema waendelea,
Wajamaa wa zamani, ubepari 'kawaoa,
Ulozi wa mkoloni, atubeba mgongoni:
Kamba akiziachia,
Lazima kuendelea !

Mijini na vijijini, uongo wakaambiwa,
Eti ndugu afkani, bado sisi wajamaa,
Wananchi wakaamini, huku wao wanazoa,
Ulozi wa mkoloni, atubeba mgongoni:
Kamba akiziachia,
Lazima kuendelea !

Vyama vingi kuadhini, ukweli nje ukawa,
Mwadanganywa wanandani, hatuna tena ujamaa,
Ubepari twaamini, viongozi wanshakua,
Ulozi wa mkoloni, atubeba mgongoni:
Kamba akiziachia,
Lazima kuendelea !

Watu hawakuamini, wakadhani wataniwa,
Kufika 'spitalini, shilingi wakadaiwa,
Nayo haionekani, inakimbia bondeni,
Ulozi wa mkoloni, atubeba mgongoni:
Kamba akiziachia,
Lazima kuendelea !

Kurejea mashuleni, ada haikuwahadaa,
Kasema nami toeni, mwatoka msipotoa,
Mikono ikawa kichwani, kila mtu analia,
Ulozi wa mkoloni, atubeba mgongoni:
Kamba akiziachia,
Lazima kuendelea !

Kaondoka mkoloni, mweusi tuliyemjua,
Huyu wetu wa hisani, mweusi kama mkaa,
Na rohoni na moyoni, ndivyo aliyozaliwa,
Ulozi wa mkoloni, atubeba mgongoni:
Kamba akiziachia,
Lazima kuendelea !

Mazuri ayatamani, kwake na wanawe pia,
Ila siwe mwanagani, babayo asiyemjua,
Na wengi wetu nchini, mayatima tumekuwa,
Ulozi wa mkoloni, atubeba mgongoni:
Kamba akiziachia,
Lazima kuendelea !
   

No comments: