Tuesday, June 12, 2012

Y A M U Y A M U P E D E J H E E !

NGOJA niwasimulie, mengi msiyoyajua,
Ili kesho msilie, eti hamkuambiwa,
Dunia usiitanie, ni shushu umeumbiwa,
Yamuyamu pedejhee, nyamunyamu moto pia !

Dunia usiidhanie, ni rafiki wa kufaa,
Ni pai umgundue, mambo atahadithia,
Kizimbani uingie, ushahidi akatoa,
Yamuyamu pedejhee, nyamunyamu moto pia !

Sikia niwaambie, kitu hatosingizia,
Ila yote ayatoe, ukweli tupu ukawa,
Pakwenda usipajue, ukabaki unalia,
Yamuyamu pedejhee, nyamunyamu moto pia !

Tamu tamu pedejhee, puani utakitoa,
Motoni uungulie, moto mali yako kuwa,
Haya yangu uchungue, dhihaka kutofanzia,
Yamuyamu pedejhee, nyamunyamu moto pia !

Usiache 'kunogee, pepo ukaidhania,
Ni matete yatetee, kiziwi kutosikia,
Ni tambaa liondoe, upofu kutoingia,
Yamuyamu pedejhee, nyamunyamu moto pia !

Na mja ujitambue, kwanini umezaliwa,
Haukuja ufukiwe, chochote kutojaliwa,
Machoni uondolewe, utupu ukabakia,
Yamuyamu pedejhee, nyamunyamu moto pia !

Anisi uzingatie, kiumbe kujitambua,
Vingine huja isiwe, uishi umeishiwa,
Na kitanzi ujitie, taabu kutovumilia,
Yamuyamu pedejhee, nyamunyamu moto pia !

NI hadithi muijue, adili iliyojaa,
Na wajinga wazingue, simulizi kukataa,
Mpaka yawafikie, wenzi wakasimuiia,
Yamuyamu pedejhee, nyamunyamu moto pia !

Ibakie hatimaye, na laiti ningejua,
Kikaingia kiwewe, dhiki unaowaachia,
Wabondwe wasibandue,  viraka vya kufulia,
Yamuyamu pedejhee, nyamunyamu moto pia !

No comments: