Thursday, June 14, 2012


Mama kakwambia kweli ?

AKILI wasiopewa, ujanja huutumia,
Yake kuwa, huwagawa, tena pasi kujijua,
Akawa achekelea, wajinga mlivyokuwa,
Mama kakwambia kweli, au huna ujualo ?

Ndio nakuulizia, kama hili unajua,
Wengi huwa wabomoa, sana watu kama hawa,
Tena mkubwa udhia, nyumbani wanapokuwa,
Mama kakwambia kweli, au kesha kupotosha ?

Huru ukiwaachia, hawana demokrasia,
Udikteta huzua, waliko kujivutia,
Kuachia hukataa, hata wakikataliwa,
Mama kakwambia kweli, au huna ujualo ?

Huzua wanayozua, na uongo kuutia,
Na aibu wala haya, kamwe hawakujaliwa,
Moto wanauhofia, lakini wasogelea,
Mama kakwambia kweli, au kesha kupotosha ?

Wazuri wa kutumia, hata mnapoishiwa,
Nderemo yao nazaa, na kesho yao mafua,
Mazuri huyakimbia, wakavamia mabaya,
Mama kakwambia kweli, au huna ujualo ?

Kawaida humtokea, ila sio mazoea,
Na mitume nao pia, haya wanasimulia,
Mwema unapozaliwa, zawadi yako mbaya,
Mama kakwambia kweli, au kesha kupotosha ?

Ni nani kakuambia, baba aweza kujua,
Hii ni ngumu sheria, yashinda wanasheria,
Si Mchagga ungeria, ndio kwanza ukatoa,
Mama kakwambia kweli, au huna ujualo ?

Masikio watakiwa, vyema ukayatumia,
Kila unalosikia, usiache kuchungua,
Ukweli unafukiwa, watakiwa kufukua,
Mama kakwambia kweli, au kesha kupotosha ?

Wapo walio vichaa, tayari wamewazaa,
Nje hutomdhania, ila kwa ndani yakawa,
Kiatu kinachopwaya, guu kinaliachia,
Mama kakwambia kweli, au huna ujualo ?

Twavaa zetu kofia, uongo zilizojaa,
Humjui, akujua, ndivyo ilivyo dunia,
Hushikwa wasiokuwa, na walo wakaachiwa,
Mama kakwambia kweli, au kesha kupotosha ?

Wapo wanayoyavaa, mawani yao ya jua,
Na rangi iliyokuwa, nakshi ikaitia,
Nyeusi iliyokua, na vitu kuwapotea,
Mama kakwambia kweli, au huna ujualo ?

Kama kasha ingekuwa, mioyo tukafungua,
Mengi tungejionea, ambayo hatujaambiwa,
Na hii ndiyo dunia, mengi hatutayajua,
Mama kakwambia kweli, au kesha kupotosha ?


No comments: