Tuesday, June 12, 2012

Sultani Jettha njaa




ULAFI umewajaa, kiu chao cha dunia,
Ni jangwa yao njaa, ukubwa iliyokuwa,
Kila kitu wachukua, kukomba na kufagia,
Kila kitu wajilia, njaa wanatuachia !

Sultani Jethwa njaa, matandu anachukua,
Azikomba sufuria, hadi safi zinakuwa,
Na harufu ajilia, hakuna chakubakia,
Kila kitu wafukia, njaa wanatuachia !

Uroho umemjaa, ulimwengu atumbua,
Milioni vitumbua, maandazi kwa gunia,
Si wilaya si mkoa, hakuna la kubagua,
Kila kitu wajilia, njaa wanatuachia !

Inda inamsumbua, vyote anafakamia,
Kukwamwa kutohofia, macho akayokodoa,
Na watu awashangaa, yeye kumwajabikia,
Kila kitu wafukia, njaa wanatuachia !

Minofu wainyofoa, vya mwanzo  wakajilia,
Mifupa wakafumua, kinywani kujisagia,
Yote yakashindiliwa, pasiwe cha kusalia,
Kila kitu wafukia, njaa wanatuachia !

Makombo hutoyajua, nao hao ukikaa,
Viporo wavikamia, kila vinapotokea,
Sembuse ule kipya, cha leo kupakuliwa ?
Kila kitu wafukia, njaa wanatuachia !

Achimbua masinia, kama Ngorongoro kuwa,
Visahani apakua, tumboni vikaishia,
Na ndoa anajinywea, tone kutokusalia,
Kila kitu wafukia, njaa wanatuachia !

Sultani Jettha kawa, kwa mito kuibugia,
Na maziwa ajinywea, katu hatohurumia,
Bahari ikibakia, kesho ataitumia,
Kila kitu wajilia, njaa wanatuachia !

Husuda imemtambaa, zongo hatoliachia,
Hata vinavyojifia, haramu havijakuwa,
Anatisha nakwambia, watu wanamhofia,
Kila kitu wafukia, njaa wanatuachia !

Wengi wajiulizia, njaa ikiendelea,
Haji kuwageukia, mla watu kujakuwa,
Macho kaa yanakuwa, kwa wekundu kumjaa,
Kila kitu wafukia, njaa wanatuachia !

Usiku hujiwakia, simba ukamdhania,
Yowe ukaliachia, ikazizima mitaa,
Mwenyewe ukaduwaa, washtuka wamjua,
Kila kitu wajilia, njaa wanatuachia !

Tadi imemtandaa, mtandao imekuwa,
Yaota kama tabia, na vazi ajivalia,
Huwezi kumtengua, mbali nayo akakaa,
Kila kitu wafukia, njaa wanatuachia !

Uchu unamchachua, hadi chachu ukatoa,
Chachandu akazitwaa, kinywani kushindilia,
Hata kavu  huvamia, hivyo hivyo akatia,
Kila kitu wafukia, njaa wanatuachia !

Adha wanatuachia, vijana wa Tanzania,
Kila tukifikiria, ugumu twajionea,
Kazi kweli kujiokoa, Jettha hatotuachia,
Kila kitu wajilia, njaa wanatuachia !

Njaa inaendelea, kila kitu chapungua,
Bei juu zikapaa, katika yetu mitaa,
Na shilindi wametwaa, mfukoni imekaa,
Kila kitu wafukia, njaa wanatuachia !

Jikoni wameingia, vyachemka wapakua,
Unapokitazamia, tayari wamekizoa,
Majivu yakabakia, maji yameshamwagiwa,
Kila kitu wafukia, njaa wanatuachia !

Ukabila umekua, jina jipya kutumia,
Uchama wa kuibua, na njaa kujigangia,
Hata kwa wasiojua, kujifanza wanajua,
Kila kitu wajilia, njaa wanatuachia !

Ni sanaa imekuwa, mchezo waendelea,
Kuiga na kuugua, hali ya watu ikawa,
Mifano sijaijua, na sitaki kuijua,
Kila kitu wafukia, njaa wanatuachia !




No comments: