Tuesday, June 12, 2012

Mimi sijafilisika

KWELI ninawaambia, mimi sijafilisika,
Ila ninachokijua, ni shilingi sijashika,
Mfukoni nafulia, sina la kusalimika,
Mimi sijafilisika, lakini sina shilingi !

Mbona mwaniangalia, au bado kueleweka,
Nasema sijafulia, ila nimepukutika,
Shilingi imeambaa, kwingine kutiririka,
Mimi sijafilisika, lakini sina shilingi !

Siwezi kuizuia, kila mtu aitaka,
Kila nikiimbilia, mwengine anaidaka,
Tupu ninaambulia, na jasho  kumiminika,
Mimi sijafilisika, lakini sina shilingi !

Shilingi yanitania, mara nyingi naponzeka,
Imezidsha hadaa, hapa kwetu Tanganyika,
Nd'o ma'na Tanzania, wapo tunaoitaka,
Mimi sijafilisika, lakini sina shilingi !

Wameificha kubaya, tena kusikofikika,
Wenyewe wanakujua, fisadi wakusifika,
Ukiritimba wazua, ni wao tu kuishika,
Mimi sijafilisika, lakini sina shilingi !

Tumebakia tamaa, kuzidi kuathirika,
Mifufko mitupu yawa, kwa siku kutaabika,
Kama gari kushtua, linabidi kufanyika,
Mimi sijafilisika, lakini sina shilingi !

Vishilingi tunalia, mashilingi wanacheka,
Na bado twakamuliwa, ili yao kujengeka,
Hupewa aliyejaa, asokitu yakamfika,
Mimi sijafilisika, lakini sina shilingi !

Hii ndiyo Tanzania, na wala si Tanganyika,
Laiti ingelikuwa, labda ningesalimika,
Kwa kutoa na kugawa, pengine kukapunguka,
Mimi sijafilisika, lakini sina shilingi !

No comments: