Tuesday, June 12, 2012

Nao wacheza sinema



Yabadilika dunia, wengine hawajajua,
Wanataka kama kawa, ilivyo kuendelea,
Kwa wengi huu ni udhia, wanataka kuutoa,
Nao wacheza sinema, waifilisi dunia !

Watu wajishindilia, kama dona lilokuwa,
Katika kujenga njia, matumbo kuyanyanyua,
Na wenzao waumia, kwa kiu pia na njaa,
Nao wacheza sinema, waifilisi dunia !

Bilioni wazitwaa, kwa kuiga na sanaa,
Jasho wanaolitoa, kidunchu kuambulia,
Swali sasa latembea, sababu kuitambua,
Nao wacheza sinema, waifilisi dunia !

Ni fisadi walokuwa, bei wakaziinua,
Hali zao kutanua, na vifug kuvifua,
Hakuna la kuingia, ila gharama zajaa,
Nao wacheza sinema, waifilisi dunia !

Soka ukiangalia, wakubwa walitumia,
Chumo haramu kutwaa, vya wengi wakajilia,
Na maisha ya sanaa, na anasa kuogea,
Nao wacheza sinema, waifilisi dunia !

Na sinema nazo  pia, wengi zinawaibia,
Trilioni wazitwaa, ili kwenda jichafua,
Ndio ukiangalia, yanawaua madawa,
Nao wacheza sinema, waifilisi dunia !

Na muziki nao pia, hasa wao wa Ulaya,
Fedha wanazichukua, haramu zilizojaa,
Sauti kuandalia, watu wanararuliwa,
Nao wacheza sinema, waifilisi dunia !

Mipaka wamepitua, watakiwa kwangalia,
Na nafsi kuchungua, kama haki inakuwa,
Na kama wakijijua, hili watalikataa,

Usawa unatakiwa, kugawa kinachoingia,
Isibweteke dunia, wengine kuwaachia,
Bilioni kuchukua, wengine kukosa mia,
Nao wacheza sinema, waifilisi dunia !

Haki hili halijawa, wataomba kulaaniwa,
Hasira zikiwajaa, hapa hamtapakaa,
Ni wapi mtakimbilia, msokwenda kujifia ?
Nao wacheza sinema, waifilisi dunia !

Twayataka manufaa, ya msingi kupatiwa,
Kisha watu kutumbua, na hekalu kunyanyua,
Vinginevyo twakataa, misuli tutazinoa,
Nao wacheza sinema, waifilisi dunia !

Mliua ujamaa, uroho mliojaa,
Hali fika mnajua, ubepari ni kinyaa,
Sasa mnajionea, kitu gani mwatwambia ?
Nao wacheza sinema, waifilisi dunia !

No comments: