Monday, June 18, 2012

Ni vyema kumkataa



Tabia ni mazoea, kuisha haitakuwa,
Fisadi aliyekuwa, kati hawezi achia,
Na kila mwenye kunukia, yafaa kumuambaa,
Kila anayenukia, harufu ya ufisadi:
Ni vyema kumkataa!

Utamu ukimkolea, pima ataichukua,
Hutaka jiongezea, kikubwa zaidi kuwa,
Pasiwe wa kutangulia, sifa yeye kuchukua,
Kila anayenukia, harufu ya ufisadi:
Ni vyema kumkataa!

Pasiwe na kupungua, nyuma aje kurejea,
Mbele ndo yake njia, hatotaka kuchelewa,
Pumzi akipumua, huiwazia dunia,
Kila anayenukia, harufu ya ufisadi:
Ni vyema kumkataa!

Huiwazia dunia, na yake yapate kuwa,
Mipango kutoijua, mingine kuandaliwa,
Alaa akangojea, kumnasa apajua,
Kila anayenukia, harufu ya ufisadi:
Ni vyema kumkataa!

Uuungu watajitia, na mbwembwe kukumbatia,
Hutoa na wakatwaa, na vya watu kuchukua,
Ni mabwana walokuwa, watwana wasaidia,
Kila anayenukia, harufu ya ufisadi:
Ni vyema kumkataa!

Huvua wakayavaa, watende na kutendua,
Kaya wakaziingia, na kuzitwaa hidaya,
Wakaonekana poa, kwa misaada kutoa,
Kila anayenukia, harufu ya ufisadi:
Ni vyema kumkataa!

Mashemeji wa ridhaa, na bandia walokuwa,
Na wana wa kujilia, hata nje huzaliwa,
Na asili kuijua, ngumu sana kuijua,
Kila anayenukia, harufu ya ufisadi:
Ni vyema kumkataa!

Waganga huwafumbia, giza likawasugua,
Vioo wakakimbia, ukweli vinavyotoa,
Vyoo vyao vikijaa, marashi huongezewa,
Kila anayenukia, harufu ya ufisadi:
Ni vyema kumkataa!

Na maua yakatiwa, kwa rangi za kuchagua,
Jasmini ikafaa, mawaridi nayo pia,
Ila zamu hufatia, kunuka na kunukia,
Kila anayenukia, harufu ya ufisadi:
Ni vyema kumkataa!

Fedha zinawazuzua, njaa inayosumbua,
Sasa wanunuliwa, kukitakasa kinyaa,
Heshima yawapotea, nao hawajajijua,
Kila anayenukia, harufu ya ufisadi:
Ni vyema kumkataa!


No comments: