Thursday, June 14, 2012

K I S W A H I L I N I M I Z I Z I

Kanifundisha mtunzi, Shaaban wa kusifiwa,
Lugha yetu kuienzi, na vita kupigania,
Wala nisiwe dumuzi, kuja kuimung'unyua,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Kiswahili ni mizizi, maendeleo kumea,
Nyengine ni kizuizi, hatuachi kudumaa,
Tukaukosa ujuzi, wa nchi kujijengea,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Tukadhania ulozi, tayari tunshafanziwa,
Tuwachune watu ngozi, ili kwenda agulia,
Nalo lisifanze kazi, kwani kweli haikuwa,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Wachawi ni viongozi baadhi kununuliwa,
Wasione mapinduzi, wakati unshafikia,
Wakadai hatuwezi, kumbe kitanzi watia,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Wenye mema maongozi,  China na huko India,
Hili wamelipa enzi, nchi sasa zinakua,
Sisi twafanza ajizi, twaendelea sinzia,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Malaysia siku hizi, lugha yao watumia,
Wameifanza azizi, maarifa kuyatia,
Na sasa ni wagunguzi, vitu kwao twanunua,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Vietnam wa majuzi, kilingeni waingia,
Hawartaki mashauzi, lugha yao watumia,
Sisi vijizee vya enzi, nyuma twenda kubakia,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Akili kama kunazi, yanshindwa kuingia,
Wengi ni ving'ang'anizi, kasumba imeingia,
Mzungu kawa Mwenyezi, sasa wamuabudiwa,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Hii si ya zama enzi, yabadiika dunia,
Tena sio maongezi, ila fani zatakiwa,
Kalimani wanahodhi, lugha zote kuelewa,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Dira hazifanyi kazi, mishale imepangua,
Hatwendi kwa matatuzi, twenda pasi kujijua,
Hali hii hatuwezi, kwendelea nawambia,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Nchi yataka mizizi, wenzetu mnaing'oa,
Upuzu au ujuzi, ukweli sijaujua,
Vijana hawana kazi, kwa lugha kutoijua ?
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Umezidi ulowezi, maji mnaumwaia,
Hawakai wawekezi, hawa wa kujipitia,
Hili kama si wajuzi, mtakuja angamia,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Lugha hii ya enzi, kutumia inafaa,
Tokea ya chini ngazi, hadi juu kufikia,
Na katika zetu kazi, ufalme kuchukua,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Katika yetu mazazi, hadi wana wanakuwa,
Kama China kudarizi, ni vazi kujishoneea,
Tukawa nayo mizizi, chini sana yachimbiwa,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Kiko katika ngamizi, imebaki kutumia,
Kama si yao ajizi, hili ningelisimamia,
Wajifanza wachuuzi, yao nikayaachia,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Maprofesa wajuzi, hili wamelichangia,
Na katika kila ngazi, ubingwa wametumia,
Kwa malaki wakufunzi, maneno wameng'amua,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Walikuwa chapakazi, kundi hili latimia,
Lugha yao wakaenzi, ngazi ya juu ikawa,
Wakatambua azizi, imebaki kuchanua,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

IT kumbe wezi, Ukenya ukaingia,
Hatimilki kukidhi, kidole asiyetia,
Tumemuachia Mwenyezi, yote haya anajua,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Wote wanamapinduzi, moja ilikuwa nia,
Zijeota chipukizi, kwa mashine kutumia,
Ukafanzwa uenezi, mashuleni kutumia,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Ndani wavia ujuzi, hili hawakutambua,
Wamekwama wanagenzi, pengine kwenda chimbua,
Japo ninayo machozi, sijatamani kulia,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Dhuluma zao ajizi, nia njema zimeua,
Kwao wana ubaguzi, na lugha waichezea,
Kwendeleza hawawezi, yao mengi yatavia,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Na MS yao enzi, mwisho inshafikia,
Kwa huu wao upuuzi, mkenge wameingia,
Nokia sio uuguzi, ni kazi kujinyanyua,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Budi tuwe wachukuzi, wenyewe kuyachukua,
Upya tukadarizi, ya zamani kufumua,
Na kisha mapandikizi, mema tukajipandia,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Kahigi mchapakazi, bado unahitajiwa,
Vitakwisha vizuizi, ulingoni kurejea,
Na Madumula mkwezi, nazi njoo 'ziangua,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Hatunao utambuzi, nchi imezainiwa,
Na walio kwenye enzi, lugha wanaichafua,
Bajeti ikiagua, lishindwe yapi lugha?
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Waona haina hadhi, Tanzania kutumia,
Wachina wangesikia, hakika wangezimia,
Wakajua ni majuha, wakubwa tuliokuwa,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Wakopwapi wenye mazi, shamba wakamwagilia,
Mafundi pamwe wajenzi, tumejaa Tanzania,
Tukizawadiwa uzi, mbona kufuma twajua,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Wangelijua malezi, kuwa nayo twatakiwa,
Wangeshiriki mazazi, upya kufikiria,
Na kuchangia majenzi, hadi nyumba ikakua,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Wasingefanza ajizi, lugha wakajinyongea,
Waonekane machizi, hawajaijua njia,
Wapi yaenda dunia, na lugha zinazotakiwa,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Tukipata viongozi, lugha watakaolea,
Sio ving'ang'anizi, dharau waliojaa,
Yatazuka mapinduzi, nchi ikaendelea,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Uturuki ni wajuzi, hili wamelipania,
Kila kitu watengezi, hawana cha kununua,
Wauza kama machizi, Tanzania waingia,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Pasi hili uvumbuzi, utazidi kujifia,
Wapo wasio na kazi, nchini wahujumiwa,
Mlowezi ni mkazi, wawaiza kuvumbua,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Lugha zao ni za wizi, kila kitu wachukua,
Wala kitu hutangazi, bado watakifukua,
Tahamaki ni ya juzi, tayari yanshakua,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Ili kuwa wagunduzi, lugha yetu yatakiwa,
Au ubaki ushenzi, soko la wengine kuwa,
Na majivu na masinzi, aibu yetu kujaa,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

Vinginevyo wapuuzi, vyetu vyote kutwibia,
Kabla kuanza kazi, wao wameshachukua,
Fikra mgando hizi, zitakujatuumbua,
Kiswahili ni mizizi, kama twataka kukua !

No comments: