Thursday, June 14, 2012

Kanga ovyo nimekaa

Kanga nimekasirika, kitenge kanichengua,
Bila aibu kamaka, uzuri kanizidia,
Na bei juu kaweka, siwezi kumfikia,
Kanga ovyo nimekaa, kitenge kahifadhiwa !

Akazidi kubwetuka, hata ndani aingia,
Pazuri wakamuheka, bila kusumbuliwa,
Kabatini akafika, au sandukuni kukaa,
Kanga ovyo nimekaa, kitenge kahifadhiwa !

Ila mimi sina mwaka, kila pembe natupiwa,
Ndani yanayofanyika, aibu najionea,
Heshima imetoweka, ninavydharauliwa,
Kanga ovyo nimekaa, kitenge kahifadhiwa !

Mafichoni huniweka, mwenzenu nikaugua,
Nikataka kutapika, na mbali nikakimbia,
Ila wanavyonishika, ni viumu kujiondoa,
Kanga ovyo nimekaa, kitenge kahifadhiwa !

Kidogo nikichanika, kazi nyingine napewa,
Kitenge atatibika, na kiraka kuwekewa,
Mie ninafadhaika, humo ninamoingia,
Kanga ovyo nimekaa, kitenge kahifadhiwa !

Siwezi kusetirika, ni aibu nakwambia,
Na kitenge aropoka, umbeya alivyojaa,
Hivi sasa nasifika, mhifadhi wa shubaka ?
Kanga ovyo nimekaa, kitenge kahifadhiwa !

Natamani kuokoka, vingine kuvikimbia,
Namtafuta Mayoka, na Liganga kuwambia,
Na nyumbani kutambika, kuliepuka balaa,
Kanga ovyo nimekaa, kitenge kahifadhiwa !

Mwenzenu naghadhabika, karibu kuwa kichaa,
Hakika ninaudhika, wapendavyo kunivaa,
Na waganga wanishika, na uchafu waniachia,
Kanga ovyo nimekaa, kitenge kahifadhiwa !

Wachawi wananitaka, kwa yao kunitumia,
Mzima wananizika, na chini kunifukia,
Watoto wasiotaka, yao wanipangusia,
Kanga ovyo nimekaa, kitenge kahifadhiwa !

Kitanzi nikikitaka, kibao wageuzia,
Wao wende kujizika, na mimi nikabakia,
Ninaitwa wa kuchoka, watu wanajinyongea,
Kanga ovyo nimekaa, kitenge kahifadhiwa !

No comments: