Tuesday, June 12, 2012

Mola atawapa wetu

Mwalimu twamsifia, adili alivyojaa,
Hana aliyependelea, hata wale wa kuzaa,
Wote wana tulikuwa, kwenye yetu Tanzania,
Mola atawapa  wetu, ukiwapenda wa kwako !

Wadhifa ukijaliwa, ni wote kutumikia,
Sio kuja kubagua, vyako ukapendelea,
Hili likiendelea, haitokuwa murua,
Mola atawapa  wetu, ukiwapenda wa kwako !

Watu watajionea, na wengine kusikia,
Inda wengi wakajaa, kadhalika tadi pia,
Na chuki inapowajia, si mazuri inazaa,
Mola atawapa  wetu, ukiwapenda wa kwako !

Dini ukizingatia, mipaka huangalia,
Na huwezi kujitia, zaidi ya Mola wajua,
Huyu ndiye wa kutoa, na pia ndiye hutwaa,
Mola atawapa  wetu, ukiwapenda wa kwako !

Mambo ukijipangia, yake hujipangia,
Hayawezi kuwa sawa, zaidi yeye ajua,
Ila ukimwaminia, huna kitachopotea,
Mola atawapa  wetu, ukiwapenda wa kwako !

Waweza nisingizia, wivu umeniingia,
Ila nianchotambua, daawa ninaitoa,
Ya wengi kuja wafaa, wala si mtu mmoya,
Mola atawapa  wetu, ukiwapenda wa kwako !

Ninakuomba Jalia, wako mwema msamaha,
Kiumbe twatarajiwa, sikuzote kukosea,
Si kamili tulokuwa, nawe hili unajua,
Mola atawapa  wetu, ukiwapenda wa kwako !

Twawaomba adilia, kesho wanaoitambua,
Mambo wakapangilia, wewe upo wakijua,
Si wao kujifanyia, kimiungu wa dunia,
Mola atawapa  wetu, ukiwapenda wa kwako !

No comments: