Tuesday, June 12, 2012

Nani kama Tanzania



KAMA njugu tunagawa, vilemba nazo kofia,
Madeni tumeridhia, kulipwa inatakiwa,
Na wakati unafaa, wengine kuwakomoa,
Nani kama Tanzania, zawadi tunavyogawa!

Kwetu huu ushajuaa, tena ni kubwa sanaa,
Chenga tunavyochengua, na harusi kuwatia,
Wababaika raia, goli zazidi ingia,
Nani kama Tanzania, zawadi tunavyogawa!

Ikulu tukianzia, hupanga na kupangua,
Na wababe walokuwa, pazuri hupachafua,
Palipooza kufaa, na shilingi kuelea,
Nani kama Tanzania, zawadi tunavyogawa!

Nchi kama ya majuha, sio ghali kuhadaa,
Huchimba ukachimbua,wakadhai yawafaa,
Hupanga na kupangua, malengo yakapotea,
Nani kama Tanzania, zawadi tunavyogawa!

Huvaa kisha kuvua, bado uchi wabakia,
Huongeza ukatoa, wakadhani yamekuwa,
Yakawa yasiyokuwa, yalokuwa, kutokuwa,
Nani kama Tanzania, zawadi tunavyogawa!

Ndio maana kwa mikoa, na hizo zake wilaya,
Watu wanakazania, madaraka kugawiwa,
Wenyewe wakachaguaH, na wala si kuchaguliwa,
Nani kama Tanzania, zawadi tunavyogawa!

Hupandwa kisichomea, na dhahiri hujifia,
Eneo kutoendelea, likawa linasinyaa,
Mla anajinapatia, atawajali waliwa?
Nani kama Tanzania, zawadi tunavyogawa!

Hupaa wasiopaa, wakatua  wasotua,
Paka akiota mbawa, mbona ndege watalia,
Kila wanapogundua, yuko nyuma awajia,
Nani kama Tanzania, zawadi tunavyogawa!

Nani atakayekataa, bure anachokipewa,
Kula ni yetu tabia, lakini sio kuzaa,
Ndiyo hayo majaliwa, kila mtu ayajua,
Nani kama Tanzania, zawadi tunavyogawa!

Wanena kuhadhithiwa, wapo wanaojionea,
Giza lishatokomea, katika yetu dunia,
Mwanga sasa unapaa,  hata tusikokujua,
Ipi kama Tanzania, zawadi tunavyogawa!


No comments: