Tuesday, June 12, 2012

Imani ya kweli dawa



Naam, kuna kulia, kadhalika na kucheka,
Kiumbe hunyanyuliwa, na pengine kuanguka,
Shiriki wanaokataa, waombayo yanafika,
Imani ya kweli dawa, ukiomba unaponya !

Ya kwao yakawa dawa, hata watu kuponyeka,
Mkeka waliolalia, wakaweza kunyanyuka,
Na majamvi ya wafiwa, yasiwe yanakunjuka,
Imani ya kweli dawa, ukiomba unaponya !

Viwete wakatembea, pasi mkongojo kushika,
Uzee walioingia, migongo ikanyanyuka,
Ujana kujisikia, yao tena kufanzika,
Imani ya kweli dawa, ukiomba unaponya !

Daima waliolia, siku moja wakacheka,
Majuma waliosinzia, wakaanza kuamka,
Mwezi waliougua, magonjwa wakatibika,
Imani ya kweli dawa, ukiomba unaponya !

Hii tiba maridhawa, , maradhi yakikufika,
Husafisha na kutoa, nawe ukasalimika,
Pumzi zikarejea, na kuondoka mashaka,
Imani ya kweli dawa, ukiomba unaponya !

Tatizo likikujia, kwayo hii kutosheka,
Huwa linatatuliwa, ukatoweka wahaka,
Maisha yakatulia, mambo yako kujengeka,
Imani ya kweli dawa, ukiomba unaponya !

Epuka wanaopotoka, ubora wakajitia,
Ujanja wakauteka, ujao kuwapindua,
Wengine wakiwazika,  kumbe wanajifukia,
Imani ya kweli dawa, ukiomba unaponya !

Viongozi wa mashaka, wanoponzeka kwa njaa,
Wakaua jumuiya,  vijisenti kuvishika,
Wapatie hii dua, yote yanaporomoka,
Imani ya kweli dawa, ukiomba unaponya !

Watu wasiotosheka, dhukuma wakaingia,
Wape bila ya mipaka, nawe mbali ukakaa,
Vituko vitawafika, katika hii dunia,
Imani ya kweli dawa, ukiomba unaponya !

Ama wanaokuweka, dunia huwanyanyua,
Machozi 'kibubujika, viganya vikaondoa,
Ukawa warehemeka, moyo wako ukatua,
Imani ya kweli dawa, ukiomba unaponya !



No comments: