Tuesday, June 12, 2012

Ufalme wa mabaa



Ya Wahabu yamekua, eneo kuangamia,
Zawadu wanayopewa, maisha kuyachafua,
Na chama chatuhumiwa, mstari wa mbele kuwa,
Ufalme wa mabaa, na taji la changudoa:
Chama kimetuvalisha,
Tabata twavijutia !

Mabaa yanazaliwa, uharamu yalojaa,
katikati ya mitaa, waja yakawasumbua,
Utitiri umekuwa, na wazidi kuzagaa,
Ufalme wa mabaa, na taji la changudoa:
Chama kimetuvalisha,
Tabata twavijutia !

Eti cafe zimekuwa, adabu pasipokuwa,
Na uchafu umejaa, rangi uzuri watia,
Chavumiliwa kinyaa, mwananchi aumia,
Ufalme wa mabaa, na taji la changudoa:
Chama kimetuvalisha,
Tabata twavijutia !

Vilabu vinazaliwa, kaziye kutulabua,
Uzee tuloingia, twashinda kujilalia,
Dua tukajisomea, asubuhi kuingia,
Ufalme wa mabaa, na taji la changudoa:
Chama kimetuvalisha,
Tabata twavijutia !

Na watoto wanalia, kelele zawasumbua,
Mchanganyiko umekuwa, nao wote wa mafua,
Hii ndiyo Tanzania, pabaya twaelekea,
Ufalme wa mabaa, na taji la changudoa:
Chama kimetuvalisha,
Tabata twavijutia !

Makoja twajivalia, vibaka na changudoa,
Mitaani wazagaa, nusu uchi wajichua,
Wachuna na kuchanua, ni sinema imekuwa,
Ufalme wa mabaa, na taji la changudoa:
Chama kimetuvalisha,
Tabata twavijutia !

Hospitali zaugua, karibu zilizokuwa,
Na shule nazo pia, afya yao yapungua,
Nani wa kuangalia, na hii ndiyo Tanzania,
Ufalme wa mabaa, na taji la changudoa:
Chama kimetuvalisha,
Tabata twavijutia !

Macho yanajionea, viongozi walokuwa,
Mazuri wayadhania, na kundini waingia,
Au shea wamepewa, hakuna anayejua,
Ufalme wa mabaa, na taji la changudoa:
Chama kimetuvalisha,
Tabata twavijutia !

Kiburi kimewajaa, na sheria zalemaa,
Mimi ninavyotambua, kimya kuwa zatakiwa,
Kelele ndani kwishia, si mitaani kusambaa,
Ufalme wa mabaa, na taji la changudoa:
Chama kimetuvalisha,
Tabata twavijutia !

Nani wa kumlilia, viziwi waliokuwa,
Wenyewe wanatakiwa, wakubwa kujionea,
Na kisha kujifikiria, kama wao wangekuwa,
Ufalme wa mabaa, na taji la changudoa:
Chama kimetuvalisha,
Tabata twavijutia !

Kama wao wangekuwa, wangeweza vumilia,
Na wana wakalea, salama wakabakia,
Au changu watakuwa, na vibaka kuishia ?
Ufalme wa mabaa, na taji la changudoa:
Chama kimetuvalisha,
Tabata twavijutia !

Mola tunamuachia, juu sana alokuwa,
Kila kitu huanzia, na mwisho wake ukawa,
Zisikie zetu dua, nafuu twaingojea,
Ufalme wa mabaa, na taji la changudoa:
Chama kimetuvalisha,
Tabata twavijutia !


No comments: