Tuesday, June 12, 2012

Rangi yangu Mwafrika

Rangi hii yapendeza, wivu wanaionea,
Maalum katengeza, Muumba juu radhia,
Kila kitu yakiwaza, hali tuli yatulia,
Rangi yangu Mwafrika, sintoacha kuringia !

Ni sisi tunaojikwaza, hasira tukiingia,
Yao wanayoeleza, ishara hayajattoa,
Na ubora naeleza, ni uchamungu sikia,
Rangi yangu Mwafrika, sintoacha kuringia !

Rangi hizi zaangaza, mithili yake maua,
Mwenyezi kazisambaza, tofauti kuzitia,
Hana alicholemaza, uduni akautia,
Rangi yangu Mwafrika, sintoacha kuringia !

Kwa rijali na ajuza, rangi hii hutulia,
Ni kazi kuichakaza, menyewe utaumia,
Kwa alivyoipuliza, hddi ikawa yang'aa,
Rangi yangu Mwafrika, sintoacha kuringia !

Na aliowajalia, mafuta wayakataa,
Maji wakishayatia, yenyewe inachanua,
Mzungu gele kajaa, akaitia nazaa,
Rangi yangu Mwafrika, sintoacha kuringia !

Jua kazi kuunguza, mwangawe unarejea,
Kama mwangi waagizwa, utokako kurudia,
Na joto kulipunguza, ubaridi ikatia,
Rangi yangu Mwafrika, sintoacha kuringia !

Kwenye baridi hucheza, mara ikishauzoea,
Kuzizima huwa viza, hutoka wazi kifua,
Wakaona miujiza, ndani wanaougulia,
Rangi yangu Mwafrika, sintoacha kuringia !

Mushawari kaagiza, hili bora lake ua,
Toka tokea dunia, huru alipoachia,
Kweusi ilitokea, asili iliyoumbiwa,
Rangi yangu Mwafrika, sintoacha kuringia !

Kizazi kakiagiza, ufalme kuutwaa,
Wenyewe wajipunguza, wala si kwa kuridhia,
Imeandikwa najuza, mwisho wao kufikia,
Rangi yangu Mwafrika, sintoacha kuringia !

Imani ataikuza, Afrika ikajaa,
Viumbe wasojikweza, udhalili kujitia,
Dunia watatangaza, ndio watakaoachiwa,
Rangi yangu Mwafrika, sintoacha kuringia !

Kizazi ataeneza, hata watapokataa,
Yazuke wasiyoweza, ila Mwafrika kuwa,
Milenia kumaliza, haya mtajionea,
Rangi yangu Mwafrika, sintoacha kuringia !

No comments: