Monday, June 18, 2012

Miongoni mwa fisadi

WAKOLONI wamekuwa, nchi tuliowaachia,
Yalayale yalokuwa, ndio wameyakamia,
Ni kuganga yao njaa, na nchi  kuachilia,
Nani mwenye uzalendo, miongoni mwa fisadi ?

Mkoloni amekuwa, mweusi aliyekuwa,
Mweupe kawaachia, nao wanayatumia,
Huu mkubwa udhia, pale wanaponunuliwa,
Nani mwenye uzalendo, miongoni mwa fisadi ?

Kila kona natembea,  hata chini kufukua,
Chama sijashuhudia, cha wazawa kubakia,
Vyama vimenunuliwa, na tajiri mujiria,
Nani mwenye uzalendo, miongoni mwa fisadi ?

Watu vinawaibia, kwa kushoto na kulia,
Hazina wazivamia, na cha watu kuondoa,
Na kodi wakichukua, wajua wanavyotumia,
Nani mwenye uzalendo, miongoni mwa fisadi ?

Mishahara wanyanyua, waheshimiwa kung'aa,
Matumbo wanajazia, hakuna cha kupungua,
Huku watu wafa njaa, na bei juu zapaa,
Nani mwenye uzalendo, miongoni mwa fisadi ?

Neema wajigawia, mfukoni wakatia,
Mali kujilimbikizia, bilauri zimejaa,
Sasa wanajimwagia, wenyewe kujichafua,
Nani mwenye uzalendo, miongoni mwa fisadi ?

Fisadi wameingia, hazina wanabomoa,
Kilichomo kuchukua, vyama kwenda kuvifaa,
Kidogo huvipatia, kingi wao kuchukua,
Nani mwenye uzalendo, miongoni mwa fisadi ?

Dala tunaisikia, na dola twaitambua,
Milango walofungua, mbona wote twawajua,
Hazina wakaachia, kilichomo kuibiwa,
Nani mwenye uzalendo, miongoni mwa fisadi ?

Akili watuchezea, kwaa vijisenti kupewa,
Fikra wameishiwa, ujanja wanatumia,
Uongo sasa wazaa, na ni kazi yao kuulea,
Nani mwenye uzalendo, miongoni mwa fisadi ?

Dhahabu wameachia, wazungu waichukua,
Na ajabu ilokuwa, ni pipi walipokea,
Kila mtu ashangaa, muflisi tumekuwa,
Nani mwenye uzalendo, miongoni mwa fisadi ?

Miradi wakiandaa, ni pasenti kupatiwa,
Tena mingi imejaa, mingi yajaa udhia,
Kazi kubwa kutwibia, ili wao kutumbua,
Nani mwenye uzalendo, miongoni mwa fisadi ?

Mazao yanapotea, na kilimo chafifia,
Hawa ukiwafatia, mwisho mbaya watujia,
Na linalotakiwa, mikakati kuamua,
Nani mwenye uzalendo, miongoni mwa fisadi ?

Maradhi yanaenea, kama mwanzo kuanzia,
Watoto wanajifia, kwashakoo kuvamia,
Na bongo zinafifia, elimu yawakataa,
Nani mwenye uzalendo, miongoni mwa fisadi ?

Elimu wanaiua, na ushindani kupwaya,
Kila kitu twanunua, toka kwa waliojaliwa,
Sisi soko tumekua, kila kitu kutupiwa,
Nani mwenye uzalendo, miongoni mwa fisadi ?

Mikakati walozua, masikini wazidia,
Badala ya kupungua, hivi sasa waenea,
Maana wanaojifaa, ni wenyewe wajijua,
Nani mwenye uzalendo, miongoni mwa fisadi ?

Uzalendo waniishia, kwa uongo kukataa,
Hawa wanaoututania, sidhani wanajijua,
Kazi kwao itakuwa, wakija kujitambua,
Nani mwenye uzalendo, miongoni mwa fisadi ?

No comments: