Tuesday, June 12, 2012

Watu ukiwahadaa



NI mkono wenye haki, lake budi kutimia,
La shari haushiriki, wala heri kujapwaya,
Yake yote stahiki, daima inavyokuwa,
Watu ukiwahadaa, wako watazainiwa!

Watu hawadhulumiki, kuna toa na kutwaa,
Ifanye hiyo mikiki, leo ukaambulia,
Wana mbali hawafiki, nao watadhulimiwa,
Watu ukiwahadaa, wako watazainiwa!

Cha mtu hakiibiki, ukweli ninakwambia,
Uizi ukiafiki, kesho yako angalia,
Mjukuu hamiliki, hicho utakachokitwaa,
Watu ukiwahadaa, wako watazainiwa!

Kwa urafiki au chuki, watu ukiwahadaa,
Deni mbali halivuki, wanao yatawatukia,
Wakutwe na wazandiki, lengo likawapotea,
Watu ukiwahadaa, wako watazainiwa!

Kiumbe hadhulumiki, hili kaa ukijua,
Fanza wako unafiki, mabaya kumzulia,
Nawe mbali haufiki, hufikwa ukashangaa,
Watu ukiwahadaa, wako watazainiwa!

kaipigeni miswaki, harufu kuziondoa,
Mambo yenu unafiki, hali ukweli mwaujua,
Lakini hadanganyiki, mkweli anayejua,
Watu ukiwahadaa, wako watazainiwa!

Maisha ni mamluki, kila mtu hununua,
Ya kheri ukiafiki, maovu hukuambaa,
Ubaya ukiashiki, balaa huzinunua,
Watu ukiwahadaa, wako watazainiwa!

Nisemayo sidhihaki, japo mnayatania,
Hadi ujapo mkuki, wa Ziraili kukwingia,
Ndipo utatahamaki, hivi kweli inakuwa,
Watu ukiwahadaa, wako watazainiwa!



No comments: