Tuesday, June 12, 2012

Thamani yao hupungua



Sekula na wasokuwa, hivi sasa ni bidhaa,
Viongozi wasofaa, kundini wamejitia,
Mbwa mwitu walokuwa, ukondoo kujitia,
Hakika mnunuliwa, thamani inapungua.

Siasa zawainua, shushu kuwasaidia,
Vitini wakaingia, akili wasiokuwa,
Yao wakajifanzia, waharibu jumuiya,
Hakika mnunuliwa, thamani inapungua.

Wakubwa huwatumia, 'doomati ' wamekua,
Viatu kupangusia, ndani wanavyoingia,
Makombo wakangojea, kujenga so'walokuwa,
Hakika mnunuliwa, thamani inapungua.

Kichwani zimepungua, matumbo wafikiria,
Si wa juu wala jaa, ila ni kubwa baa,
Kila walipoingia, hakuna kuendelea,
Hakika mnunuliwa, thamani inapungua.

Mzaha na kizaazaa, uongozi wao huwa,
Ovyo kujiamlia, na ukweli kukataa,
Mishipa ikawajaa, na mapafu kupanua,
Hakika mnunuliwa, thamani inapungua.

Mola huwaangalia, huku anachekelea,
Viboko akawatia, duniani kuanzia,
Usugu wakijitia, zaidi yanawajia,
Hakika mnunuliwa, thamani inapungua.

Nguo atajawavua, hadharani wamekaa,
Kwa watu kuabudia, na shiriki kuitia,
Nami nawangong'onezea, wallahi li njiani lajaa !
Hakika mnunuliwa, thamani inapungua.

Sinema mtajionea, wa juu aliyekuwa,
Nao wanaofuatia, yake wakamfanzia,
Ngoma tete imekua, mawe hawatokimbia,
Hakika mnunuliwa, thamani inapungua.

Mali imewahadaa, hata wakfu kunyoa,
Mijeledi nasikia, Ramadhani haijawa,
Rajabu jawabu kua, tayari laandaliwa,
Hakika mnunuliwa, thamani inapungua.

Natetema kuhofia, laiti wangeelewa,
Haya kuyaangalia, mtu huwezi balaa,
Hata nani ungekuwa, nashauri kukimbia,
Hakika mnunuliwa, thamani inapungua.

Hapanayo manufaa, alojuu kumchezea,
Wenyewe mtaumia, mbaki mwagaagaa,
Na hisabu aijua, siku yenu kutimia,
Hakika mnunuliwa, thamani inapungua.

Huruma nawaombea, kwalo hili kufunua,
Kalamu nimeitwaa, taarifa kuzitoa,
Langu sikulihofia, ila yao nahofia,
Hakika mnunuliwa, thamani inapungua.

No comments: