Saturday, June 2, 2012
Mtaji wa masikini
Wajanja wamewanyoa, nguvu zenu kusifia,
Walijua ni majuha, hayo mtayasikia,
Benki wakaiachia, fisadi kuivamia,
Mtaji wa masikini, benki kuu ya taifa !
Nia yao hao mbaya, na hili wanalijua,
Milango waliachia, makusudi nadhania,
Yao yalipotimia, mifuko yao yajaa,
Mtaji wa masikini, hazina ya serikali !
Kiu nilikisikia, nikashindwa kujinywea,
Mbona sana nawajua, na mtumwa nilikuwa,
Macho nilipofungua,nikauona udhia,
Mtaji wa masikini, benki kuu ya taifa !
Mwana nilimdhania, nyayo atafuatia,
Nyuma kuangalia, yake ameshayazua,
Na kilio cha kuliwa, leo kipo Tanzania,
Mtaji wa masikini, hazina ya serikali !
Maneno kayapindua, fukara kumgeuzia,
Na kamba akamtia, ukapa ukamjaa,
Hadi leo analia, nani wa kumwangalia,
Mtaji wa masikini, benki kuu ya taifa !
Masikini azidiwa, mgongo kujipindia,
Fisadi anachukua, wakubwa kuwakatia,
Fukara kufikiriwa, ndio mwisho wa dunia,
Mtaji wa masikini, hazina ya serikali !
Walonacho wanapewa, wasonacho waumia,
Baituli mali mbaya, haifai wenye njaa,
Kadhi kawakatalia, tena mbali potelea,
Mtaji wa masikini, benki kuu ya taifa !
Adili ingelikuwa, masikini kwenda pewa,
Ndiye yeye mhitajia, tena mwenye kubwa njaa,
Mbegu akaitumia, umaskini kupungua,
Mtaji wa masikini, hazina ya serikali !
Ungekuwa ujamaa, mashamba kujilimia,
Na viwanda kuibua, pamoja kuangalia,
kama Uchina ikawa, sio sasa vyajifia,
Mtaji wa masikini, benki kuu ya taifa !
Na wanaojisheua, mwapaswa kwenda wavaa,
Ukweli wakaujua, si wajinga mlokuwa,
Ila neno latimia, wote mlioandikiwa,
Mtaji wa masikini, hazina ya serikali !
Mtaji kuugombea, na mengine kukataa,
Vijiji kuvinyanyua, na masikini kupaa,
Ufukara twauvaa, viongozi kutofaa,
Mtaji wa masikini, benki kuu ya taifa !
Mikono nainyanyua, dua yangu kuitoa,
Wengi ninawaombea, kidogo tu kujaliwa,
Shida kuwapungua, na nchi kuifurahia,
Mtaji wa masikini, hazina ya serikali !
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment