Saturday, June 2, 2012

Nampenda, anipenda



ULEVI ukiingia, wa kupenda ulokuwa,
Rahisi kuzainiwa, ukweli ukadhania,
Ndiyo ninayasikia, na asili ninaijua,
Nampenda, anipenda, hivi kweli unajua ?

Binti leo kashupaa, anapendwa kujitia,
Rijali kashuhudiwa, vingine hawezi kuwa,
Ila nimeshtukia, hili kweli halijawa,
Nampenda, anipenda, hayo unayaamini ?

Rijali wa kutumia, sio wa kushikiliwa,
Na kila mchanganyikiwa, haweshi kuhadaiwa,
Njia wakishapotea, hujidai waijua,
Nampenda, anipenda, uko wazi  moyo wake ?

Sijui wa kumjua, mmoja aliyekuwa,
Kupenda akaishia, naye aliyeanzia,
Wengi chungu huchukua, hadi juu kikajaa,
Nampenda, anipenda, au wengi awapenda ?

Katika panga pangua,  hujui litalokuwa,
Wajanja hutangulia, mbegu wakazichukua,
DNA wakitwaa, ndoa si yako, yao huwa,
Nampenda, anipenda, hivi kweli unajua ?

Mchezo hukuchezea, wazazi ukachukia,
Huyo ukamdhania, mkombozi kwao kawa,
Lao wakijipatia, haraka hukukimbia,
Nampenda, anipenda, hayo unayaamini ?

Ukabakia kulia, kujuta ulikijua,
Na sasa kujinasua, peke yako kubakia,
Wazazi wametulia, matokeo wayajua,
Nampenda, anipenda, uko wazi  moyo wake ?

Tunzo nimewaachia, ndogo sana ilokuwa,
Ila itayowaiangia, hadhari watachukua,
Bikira huvumilia, nadra kumzuzua,
Nampenda, anipenda, au wengi awapenda ?

No comments: