Saturday, June 2, 2012
Nimeumbwa kwa udongo
Sikuumbwa kwa uongo, nimeumbwa kwa udongo,
Tanzania sio Kongo, kwenye nyumba sio pango,
Mkamilifu maungo, roho pia na ubongo,
Nimeumbwa kwa udongo, sikuumbwa kwa uongo !
Na hata bila ya bango, nimeacha kikaango,
Naketi kwenye ulingo, na habari za vitengo,
Wala siogopi zongo, mfungo sio mfungo,
Nimeumbwa kwa udongo, sikuumbwa kwa uongo !
Siwezi kubali hongo, ili niwe nami mwongo,
Nikijaribu ya gongo, utaniua msongo,
Hawezi akawa chongo, makengeza kwa uongo,
Nimeumbwa kwa udongo, sikuumbwa kwa uongo !
Siukubali tongotongo, hayo namwachia fungo,
Ardhini kwenye kingo, awezaye masimango,
Kweli wangu mviringo, dunia yangu ni ndogo,
Nimeumbwa kwa udongo, sikuumbwa kwa uongo !
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment