Thursday, December 1, 2011

Uzunguuzungu nyani...

Uzunguuzungu nyani, kwa lugha pia tabia,
Nawaona hayawani, Mzungu kumwabudia,
Lugha yenu kuwa duni, ya wengine kuringia?
Uzunguuzungu nyani, hayawani aso kwao.

Hana kwao hayawani, vya wengine huvamia,
Hata wakiwa uchi nyikani, fashioni hudhania,
Nakiona kisirani, mate ninawatemea,
Uzunguuzungu nyani, hayawani aso kwao.

Eti mbaya baniani, ila kiatu chake dawa?
Utainywaje kwinini, na mseto wasaidiwa?
Sijajua kwa yakini, ila uzungu wabwia,
Uzunguuzungu nyani, hayawani aso kwao.

Utadhani majinuni, viumbe walojaliwa,
Wenye vito na madini, wengine wajichimbia,
Kumbe wangejithamini, mitaji wangeivua,
Uzunguuzungu nyani, hayawani aso kwao.

Ndarahima abadani, haziwezi kuingia,
Ikiwa watu ni nyani, na asili wamevua,
Mzungu hawathamini, hata na Mchina pia,
Uzunguuzungu nyani, hayawani aso kwao.

Hakika huu unyani, ila wakosa mikia,
Huu ndio utu gani, kwako wewe Mtanzania,
Wajifanya afkani, ukidhani wavutia,
Uzunguuzungu nyani, hayawani aso kwao.

Vijana badilikeni, si ya jana Tanzania,
Tenda changamkieni, ya kuiga kukataa,
Mengi kuwachangieni, sura mpya kutwaa,
Uzunguuzungu nyani, hayawani aso kwao.

Wengine ni kitu gani, ila tu wamejaliwa,
Maendeleo kughani, furaha na pia sanaa,
Kila kijana akabuni, watu haihai kua,
Uzunguuzungu nyani, hayawani aso kwao.

Unayo kubwa thamni huu wetu Utanzania,
Mtatamba duniani, kila mkiutangazia,
Ya wengine yaacheni, ya kwetu kuyachukua,
Uzunguuzungu nyani, hayawani aso kwao.

No comments: