Waone wana izaya, sasa ni fotokopia,
Kuiga wamejaliwa, kama sio kulaaniwa,
Wadhani njia wajua, kumbe ndio wanapotea,
Iga huru walokua, usiwaige watumwa.
Igeni yanayofaa, asili yenu kung'aa,
Siige wapita njia, katikati huishia,
Iga linalonyanyua, na heshima ukapewa,
Iga huru walokua, usiwaige watumwa.
Iga toka kwa wazawa, mila wanazotumia,
Vitu vyao asilia, utandawazi kuvaa,
Na bora vikija kua, nchi itatengemaa,
Iga huru walokua, usiwaige watumwa.
Iga huru walokua, si watumwa kwenye baa,
Utaharibu tabia, jamii ikakutaa,
Upende Utanzania, na waenzi Watanzania,
Iga huru walokua, usiwaige watumwa.
Iga chenye manufaa, kwenye nyimbo na sanaa,
Nje watakachosifia, kazi yako kuridhia,
Na mialiko kupewa, uende kuwachezea,
Iga huru walokua, usiwaige watumwa.
Thursday, December 1, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment