Thursday, December 1, 2011

Napanda ndege mtumba

Nikifa msinililie, napanda ndege mtumba,
Wakubwa nao wapambe, wameamua kutamba,
Kwa vipi mimi nigombe, na turufu weshalamba,
Napanda ndege mtumba, nikifa msinililie!

Machozi myazuie, mkilia nitagomba,
Jeneza mlitanie, maiti mkiikomba,
Na kaburi mlichezee, wavune waliyoomba,
Napanda ndege mtumba, nikifa msinililie!

Gharama msiingie, nitupeni kwenye shamba,
Au kama litokee, niwe ninacho kihamba,
Hapo mnifukie, taifa livute kamba,
Napanda ndege mtumba, nikifa msinililie!

Na msinisikitikie, mviimbe vya kuimba,
Tanga msinifanyie, fedha wapeni wajomba,
Hitima msinisomee, mwenyewe nimeshaomba,
Napanda ndege mtumba, nikifa msinililie!

Wanasiasa msivae, kuzika sijawaomba,
Senti msinichangie, hamna nami ujomba,
Na shangazi msilie, ni bora kuja kuimba,
Napanda ndege mtumba, nikifa msinililie!

Viongozi msinisifie, wala hata kunipamba,
Mlipaswa myajue, haya yataja nikumba,
Mola awatengee, cha moto mkubwa kihamba,
Napanda ndege mtumba, nikifa msinililie!

No comments: