Thursday, December 1, 2011

Huwashinda changudoa

Huanza ni wanafunzi, kazi wakakomalia,
Huufanya ubaguzi, wadogo hukataliwa,
Wakachagua kichuzi, vizito kuviwania,
Malaya wa uongozi, huwashinda changudoa!

Rahisi hawajiuzi, ghali watanunuliwa,
Ukubwa kwao majazi, vinginevyo wadhulumiwa,
Na kupanda kwao ngazi, ndilo wanatazamia,
Malaya wa uongozi, huwashinda changudoa!

Nafusi zao bazazi, uchuro zimejaliwa,
Ndarahima ni azizi, utu utaununua,
Ni gunia la viazi, binadamu twadhania,
Malaya wa uongozi, huwashinda changudoa!

Hii ndiyo yao kazi, utakayowafumania,
Mengine hawayawezi,uhayawani balaa,
Wameshagaiwa ngozi,ila yazidi sinyaa,
Malaya wa uongozi, huwashinda changudoa!

Wameshagaiwa ngozi, ya maombi kuyatoa,
Kila siku wamaizi, yasiyo na manufaa,
Kama wajibu wa ngozi, hukithiri kupungua,
Malaya wa uongozi, huwashinda changudoa!

Umekolea ujuzi, kwa mengi wanatumiwa,
Wengine huwa ushuzi, wabaki kuvumiliwa,
Na wengi ni kama mbuzi, majani wanapatiwa,
Malaya wa uongozi, huwashinda changudoa!

Hawanalo la uzuzi, akili zimefubaa,
Hawanayo mazoezi, hoja zinawazingua,
Ya kheri kwao maudhi, aghalabu hupuuzia,
Malaya wa uongozi, huwashinda changudoa!

Wajiuza kama ndizi, ukubwa kujipatia,
Ufreshi hawauwezi, kuoza huishilia,
Ni la ngano andazi, si mchele kitumbua,
Malaya wa uongozi, huwashinda changudoa!

Wapo wanaojienzi, walokua changudoa,
Malaya wa uongozi, kamwe hawajatulia,
Kutumika kwao hadhi, hata na wanaogua,
Malaya wa uongozi, huwashinda changudoa!

Utadhani madoezi, vichaa kuitikia,
Wakawafanya azizi, majumbani kuingia,
Hutaharuki jahazi, mwambani limeingia,
Malaya wa uongozi, huwashinda changudoa!

No comments: