Wednesday, December 14, 2011

Sonara

Sonara nahujumiwa, kwa kuikosa dhahabu,
Bei inaniondoa, tena kwa kubwa ghadhabu,
Nimepigwa na butwaa, sijui la kujaribu,
Sonara nahujumiwa, kwa kuikosa dhahabu.

Kila nikiangalia, daftari za hesabu,
Kiasi hakijatimia, nakisi nairakibu,
Na sababu sijajua, ili nipate jawabu,
Sonara nahujumiwa, kwa kuikosa dhahabu.

Wateja wanikimbia, wanidhani mraibu,
Hamada nimeshakua, kuwarusha si ajabu,
Nazidi kugugumia, kitu gani kuwajibu?
Sonara nahujumiwa, kwa kuikosa dhahabu.

Sonara ninaishiwa, yanazidi masahibu,
Duka laja kunifia, maisha yawe taabu,
Nani kumtegemea, dunia hii ya dubu,
Sonara nahujumiwa, kwa kuikosa dhahabu.

Uchina naulizia, hadhari wamenijibu,
Dhahabu yetu sanaa, kutwaa usijaribu,
Wateja wakigundua, zitawapanda ghadhabu,
Sonara nahujumiwa, kwa kuikosa dhahabu.

Kwa hiyo nimeamua, kijiwe kukihatibu,
Shida kuizungumzia, wenda nipate tabibu,
Akajanisaidia, kuijua akrabu,
Sonara nahujumiwa, kwa kuikosa dhahabu.

No comments: