Mpenzi nakulilia, hawara kakuhadaa,
Kidani kununuliwa, mimi ukanikataa,
Hivi sasa ni pazia, nje hautatokea,
Dhahabu nakulilia, hawara kakuchukua!
Upara kakuhadaa, mtegoni kuingia,
Njiani kakuachia, wabaki umepagawa,
Wa kweli hujamjua, mpenzi wa kukufaa,
Dhahabu nakulilia, hawara kakuchukua!
Sura hukuangalia, kiza kilishaingia,
Sasa wamuangalia, zimwi anafanania,
Watamani kumkimbia, bawaba kakuwekea,
Dhahabu nakulilia, hawara kakuchukua!
Dhahabu ungetulia, masikio kuzuia,
Yale usingesikia, wala usingezainiwa,
Pabaya kuegemea, chini umedondokea,
Dhahabu nakulilia, hawara kakuchukua!
Nachakarika radhia, wenyewe kujiinua,
Urahisi kukuingia, mara unanikimbia,
Ya kwao hukuyajua, waliyo yadhimiria,
Dhahabu nakulilia, hawara kakuchukua!
Mamluki walokua, kila kitu huchukua,
Mashimo kukuachia, ujue utalojazia,
Hawatakusaidia, hata ujapo ugua,
Dhahabu nakulilia, hawara kakuchukua!
NI kweli nimefulia, ila haujanifaa,
Ni kinyaa umekua, ndugu unaniulia,
Kuzika sala mpya, kila leo natakiwa,
Dhahabu nakulilia, hawara kakuchukua!
Wednesday, December 14, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment