Wednesday, December 14, 2011

Dhahabu unaondoka

Dhahabu unaondoka, nini unaniachia,
Humu ndani ukitoka, kitu gani chabakia?
Naona nafilisika, sina hata pa kukaa,
Dhahabu unaondoka, mashimo waniachia?

Mwenzangu unanyanyuka, kinywaji hujalipia,
Na nje tulipotoka, sina kitu nilikwambia,
Jamaa wakinishika, mbona wataniumbua?
Dhahabu unaondoka, mashimo waniachia?

Mashimo nimeyaweka, mfukoni yalokua,
Hakuna nilichoshika, utupu umebakia,
Hata ninaponyanyuka, thumuni haitalia,
Dhahabu unaondoka, mashimo waniachia?

Mpenzi unaondoka, nani wa kunilipia,
Mwenzio nitateseka, nishinwe kujitetea,
Na yatakayonifika, wewe utalaumiwa,
Dhahabu unaondoka, mashimo waniachia?

Nashindwa kukasirika, mjinga nakudhania,
Sikujua kughafilika, hadi ulipotokea,
Natamani kukunyuka, midomo kukupasua,
Dhahabu unaondoka, mashimo waniachia?

Namhofu mstahika, juu aliyejaliwa,
Asije kuhamanika, vingine kunidhania,
Haniruhusu kufoka, ila busara kutoa,
Dhahabu unaondoka, mashimo waniachia?

No comments: