Wednesday, December 14, 2011

Dhahabu hujanambia

Wenyewe tumebakia, nieleze wangu mwenzi,
Nini kilichotokea, hadi hili fumanizi,
Kwanini ulipagawa, na kudakwa na doezi?
Dhahabu hujanambia, siri yako na viongozi!

Ni nini wamekwambia, ukafanza usikizi,
Kisha kuyazingatia, maudhui kuyaenzi,
Nini walichokugea, ukaifanya ajizi,
Dhahabu hujanambia, siri yako na viongozi!

Viongozi nawajua, dunia yao makazi,
Keshowanaikataa, wajifanya ni maswezi,
Ni watu wa kupotea, usiwafanze azizi,
Dhahabu hujanambia, siri yako na viongozi!

Na wewe hukutumia, waipate yao kazi,
Na wakishajihudumia, unakuwa huna hadhi,
Na kila ikipungua, wanakuona doezi,
Dhahabu hujanambia, siri yako na viongozi!

Unapowashangilia, wanajua yako kazi,
Ni mtu wa kutumiwa, akushinda hata mbuzi,
Chizi watakudhania, mapeni unayoenzi,
Dhahabu hujanambia, siri yako na viongozi!

No comments: