Wednesday, December 14, 2011

Muoa na muozwa....

MWAMBAJE wanaubia, ya muozwa na muoa,
Liweje kutokujua, sheria kukubalia,
Na mtolewa na mtoa, hayawani nani kawa?
Kuwadi, bwanani ndoa, mafisadi na dhahabu?

Mbia kahutubia, hakusema yake bia,
Mwekeza anakazia, ni nani kamuwekea,
Mwenye mtaji maua, ni nani humtunzia?
Kuwadi, bwanani ndoa, mafisadi na dhahabu?

Mitambo kakutambia, mkodishaji wamjua,
Tambo zikitambikiwa, matumbo hamtaumia?
Wimbo msioujua, kuimba si kuumbua?
Kuwadi, bwanani ndoa, mafisadi na dhahabu?

Akili fupi mkia, huruma hakujaliwa,
Kaziye kupapatikia, nyuma kulikobakia,
Na analo ambulia, kwenye shari huishia,
Kuwadi, bwanani ndoa, mafisadi na dhahabu?

Ni mjuvi mwenye waa, usije msogelea,
Huambukiza balaa, na nuksi kuchanua,
Na kila analopewa, huvia na kupagawa,
Kuwadi, bwanani ndoa, mafisadi na dhahabu?

Wapewa tende na halua, waiuza jumuiya,
Sakra mauti ikiwa, ni vipi utajitetea,
Huruma ninakuonea, kiumbe uliylaaniwa,
Kuwadi, bwanani ndoa, mafisadi na dhahabu?

No comments: