Wednesday, December 14, 2011

Dhahabu usisahau

BABA, mama malegea, vya rada waviachia,
Kuondoa udhia, mwana akatufukua,
Na mwisho nikubakia, thamani tusiokua,
Dhahabu usisahau, nilivyokutegemea!

Mzungu kawahadaa, Rufiji kuja kuvua,
Kumbe siri aijua, vya wao wasivyojua,
Madini yanaelea, na nyara kufukiwa,
Dhahabu usisahau, nilivyokutegemea!

Njia ya kujipenyea, hapo wajitafutia,
Na mijinga ilokua, mkenge ikaingia,
Dili kujashtukiwa, wazee wakakataa,
Dhahabu usisahau, nilivyokutegemea!

Mshairi nawajua, njia walizopitia,
Watu wa kuhurumiwa, hadaa wanatumia,
Na kinga wanawekewa, vya wizi kufurahia,
Dhahabu usisahau, nilivyokutegemea!

Kinga haitowafaa, Ziraili kiingia,
Kwa sura awatambua, siku ya kuja wavaa,
Amri wataisikia,na matumbo kuwajaa,
Dhahabu usisahau, nilivyokutegemea!

Mbele wametangulia, uzaini na hadaa,
Njia ulipopotea, kurudi haukujua,
NImebaki nangojea, ni lini utatokea,
Dhahabu usisahau, nilivyokutegemea!

Jinsi nilivyotegemea, mwenzi ungeninyanyua,
Sasa sijakuelewa, kama utafanikiwa,
Bila kuja aguliwa, mashetani kuyatoa,
Dhahabu usisahau, nilivyokutegemea!

Bagamoyo nitatua, wazee kuwaambia,
Na Tanga nitapitia, nitete na Wazigua,
Na kisha nitaingia, Sumbawanga kuwangia,
Dhahabu usisahau, nilivyokutegemea!

No comments: