Babayo mwanaizaya, dhahabu nakujutia,
Nyumba uliyozaliwa, haya haikujaliwa,
Na huruma ni sanaa,na imani ni hadaa,
Mwanadhahabu udhia, babayo mwana izaya!
Babayo kanunuliwa, kwa vichache virupia,
Nje amekimbilia, changudoa wamhadaa,
Nyumbani si wa kukaa, hiyo ni yake twabia,
Mwanadhahabu udhia, babayo mwana izaya!'
Hamada wamtania, hulewa ajitambua,
Babayo nywii hubwia, hawezi akajijua,
Kote hujapekuliwa, hana anachobakiwa,
Mwanadhahabu udhia, babayo mwana izaya!
Laana kaiambua, mtu mzima akiwa,
Wazazi hakusikia, ujinga akaamua,
Mashakani kututia, leo tunagugumia,
Mwanadhahabu udhia, babayo mwana izaya!
Mikosi inatuvaa, juuchini yatokea,
Mengine kama ruia, hata hutoielewa,
Na kila ninapokaa, mwanangu nakuwazia,
Mwanadhahabu udhia, babayo mwana izaya!
Heri nyumba ya mabua, furaha ndani ikiwa,
Kuliko orofa kuwa, iliyojaa balaa,
Laiti ningelijua, fakiri angenioa,
Mwanadhahabu udhia, babayo mwana izaya!
Imebaki kumlilia, Rahmani wa Jalia,
Viumbe kutusikia, na akatuhurumia,
Akaifungua njia, kwa ibura na masaa,
Mwanadhahabu udhia, babayo mwana izaya!
Wednesday, December 14, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment