KITU chenyewe nishai, na hakifa manufaa,
Mimi kweli sikatai, kuchimbwa kuja kataa,
Ni haki walalahoi, hoja hii kuizua,
Dhahabu mwaweza dai, isiendelee kuchimbwa!
Chile wamekinai, wawekezaji kutoa,
Argentina hai, hili pia walijua,
Na huko Shanghai, Uchina waangalia,
Dhahabu mwaweza dai, isiendelee kuchimbwa!
Ni kosa la kijinai, serikali kuvamia,
Na kisha kuweka bei, wao inayowafaa,
Machimbo wakajarai, na mapato kuyatwaa,
Dhahabu mwaweza dai, isiendelee kuchimbwa!
Mgodi mjini hauwi, vijijini inakaa,
Na watu wa kuidai, wanavijiji watakua,
Na hisa kwao si ndui, kupata wanatakiwa,
Dhahabu mwaweza dai, isiendelee kuchimbwa!
Mwaambulia mafui, thamani wanaichukua,
Kwenda kwa zao nikahi, vilivyo wakajinoa,
Wewe unakufa hai, eti bado washangaa?
Dhahabu mwaweza dai, isiendelee kuchimbwa!
Kabla nikistahi, hili mtalielewa,
Mwajifanya mna bei, watu mnawanunua,
Ni kama hamnijui, sasa nawaangazia,
Dhahabu mwaweza dai, isiendelee kuchimbwa!
Hakuna nafsi hai, mauti kuyakimbia,
Iniongozaya rai, Mtanzania bila njaa,
Na hili nitalidai, hata kaburini nikiwa,
Dhahabu mwaweza dai, isiendelee kuchimbwa!
Na chini tena sikai, vita nimeviandaa,
Tovuti naenda kuwahi, kwa muda nikahamia,
Tena hii asubuhi, salamu kuwatumia,
Dhahabu mwaweza dai, isiendelee kuchimbwa!
Masheikh wazirai, rushwa wanaopokea,
Jehanamu iwadai, siku wanapofukiwa,
Na mola anistahi, hasiri nilizojawa,
Dhahabu mwaweza dai, isiendelee kuchimbwa!
Ufisadi nakinai, matapishi nayatoa,
Na dua natuma hii, Mola kuwapatilizia,
Mapadri na walei, nao waliochangia,
Dhahabu mwaweza dai, isiendelee kuchimbwa!
Wednesday, December 14, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment