Sijaiona hekima, maamuzi kufikia,
Tulishindwaje azima, mitambo ya kufukua,
Migoi inakoroma, Ulaya hadi Asia?
Hivi twashindwa azima, mitambo kujichimbia?
Zinazunguka tuhuma, nchi inahujumiwa,
Tena na watu wazima, akili walojaliwa,
Kwa hakika zimehama, sivyo tunavyowadhania,
Hivi twashindwa azima, mitambo kujichimbia?
Si siri dunia nzima, mitambo si ya kununua,
UKitaka waazima, na kazi kujifanyia,
Ukipata ndarahima, hapo utazinunua,
Hivi twashindwa azima, mitambo kujichimbia?
Halihitaji hekima, ni busara kutumia,
Adili ikisimama, rahisi kuligundua,
Ila kama kuna njama, upofu watu hupewa,
Hivi twashindwa azima, mitambo kujichimbia?
Watu wasio rehema, nafsi huzikamua,
Afadhali yake kima, wenzake anawajua,
Na huujali ujima, kesho kuja kuwafaa,
Hivi twashindwa azima, mitambo kujichimbia?
Waliokosa neema, wenyewe wanajiua,
Hawajui waadhama, mimi ndiye yeye pia,
Ikishatoka zahama, ndipo wanapogundua,
Hivi twashindwa azima, mitambo kujichimbia?
Nimemaliza kasima, yangu nawaachia,
Mtapokuja kusoma, na kisha kuyaelewa,
Mtaamua maamuma, kusuka ama kunyoa,
Hivi twashindwa azima, mitambo kujichimbia?
Wednesday, December 14, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment