Tuesday, December 11, 2012

Ziondoeni siasa


Siasa zinachafua, michezo ikatitia,
Hizi mkiziondoa, spoti mtanyanyua,
Siasa za wenye njaa, michezo yetu zaua,
Ziondoeni siasa, michezo itastawi!

Viwanja tulichangia, wao wamevichukua,
Sasa vya kwao vimekuwa, pesa wajikusanyia,
Kisha wanajigawia, sisi kavu kubakia,
Ziondoeni siasa, michezo itastawi!

Ushauri natuoa, miji viwanja kupewa,
Hisa wakajipatia, wakazi wakichangia,
Kisha wakavifufua, vipate kuendelea,
Ziondoeni siasa, michezo itastawi!

Ushindani kuuzua, mabenki kusaidia,
Mashirika kuachiwa, udhamini kuutoa,
Sio chama kudokoa, pale pale kubakia,
Ziondoeni siasa, michezo itastawi!

Huru viwanja vikiwa, tutainua Tanzania,
Kimichezo ikapaa, viwango tukafikia,
Na vingine kuzaliwa, sasa pasipojaliwa,
Ziondoeni siasa, michezo itastawi!

Golfu tunatakiwa, ekari kuziachia,
Mameneja wakapewa, kila mji kupatiwa,
Hivi vyema tukilea, dola zitatufatia,
Ziondoeni siasa, michezo itastawi!

Formula one pia, mwanzowe unatakiwa,
Miji ikashauriwa, viwanja kuviandaa,
Haba na haba najua, kibaba kitatimia,
Ziondoeni siasa, michezo itastawi!

Tenisi tunasikia, mapesa inayovua,
Wilaya za Tanzania, muhimu kuvizindua,
Wachache wakitokea, neema itaingia,
Ziondoeni siasa, michezo itastawi!

Pikipiki zimejaa, mbio zianze ingia,
Viwanja kuviandaa, watu huko wakajaa,
Wikiendi kufurahia, na huko wanajitanua,
Ziondoeni siasa, michezo itastawi!

Baiskeli nazo pia, mbio zeendeanzishiwa,
Vyama ikiandaliwa, iwe kote Tanzania,
Ya wilaya kuanzia, hadi taifa ikawa,
Ziondoeni siasa, michezo itastawi!

No comments: