Tuesday, December 11, 2012

Kama ukubwa kutengwa

Kama ukubwa nazaa, eti juu unakuwa,
Wengine kuwa  kinyaa, wasije kukaribia,
Mimi hilo nakataa, mdogo nitabakia,
Kama ukubwa kutengwa, niache kwenye udogo!

Watu kuona kinyaa, wa chini waliokuwa,
Mkono nikakataa, hata kwa kusalimia,
Si udhu kuuzuia, ila ukubwa kukwea,
Kama ukubwa kutengwa, niache kwenye udogo!

Fukara kuwakimbia, shughulini kujitia,
Yao kutoyasikia, sembuse kusadia,
Huko sintokimbilia, hapahapa nabakia,
Kama ukubwa kutengwa, niache kwenye udogo!

Vijiji kuviambaa, ugenini kutembea,
Udongo kutoujua, na harufu ya mvua,
Usafi nikajitia, kwetu wasikoujua,
Kama ukubwa kutengwa, niache kwenye udogo!

Ndege nitajipandia, kijijini kurejea,
Hawa ilivyonijaa, ya kwao kujibebea,
Asili ninaijua, masikini kuzaliwa,
Kama ukubwa kutengwa, niache kwenye udogo!

Suti nilishazikimbia, magwanda najivalia,
Buti sawa zikakaa, kijijini kuingia,
Raha nikafurahia, kilio chao kujua,
Kama ukubwa kutengwa, niache kwenye udogo!

Matatizo kuyajua, niwe ninajionea,
Yasiwe ya kusikiwa, na wengine kuambiwa,
Madogo nikatambua, na makubwa kuhofia,
Kama ukubwa kutengwa, niache kwenye udogo!

Vyanzo nikavichagua, msaada kufuatia,
Moyoni kuyachukua, kama yangu yalokuwa,
Udhibti kuulea, mwanzo na kumalizia,
Kama ukubwa kutengwa, niache kwenye udogo!

Itanichoka dunia, kilio chao kutoa,
Katu sintotindikiwa, machozi kuyaachia,
Hadi wema wakasikia, na nafuu kuingia,
Kama ukubwa kutengwa, niache kwenye udogo!

Ninakuomba Jalia, ukubwa kuundoa,
Usio na manufaa, ila mimi kujifaa,
Yatosha ulonigea, ziada naikataa,
Kama ukubwa kutengwa, niache kwenye udogo!

Ziada naikataa, ila wengine kufaa,
Hapo nitaipokea, maajabu kuyazua,
Ikatujua dunia, fukara wa kujitakia,
Kama ukubwa kutengwa, niache kwenye udogo!

No comments: