Saturday, December 29, 2012

Asali hii si tamu



ASALI hii bandia, tayari nimeijua,
Utamu haijaliwa, ila mate yautia,
Kwa hili kuling'amua, debe ninalikataa,
Asali hii si tamu, mate yanakuchezea!

Gairo naelekea, yangu kwenda kununua,
Singida nikapitia, viwango kujipimia,
Halisi nikiijua, ndio pochi kuachia,
Asali hii si tamu, mate yanakuchezea!

Asili inapokuwa, dawa kweli inakuwa,
Maradhi kujitibia, elfu yaliyokuwa,
Si uongo nawambia, kwa kila mwenye kujua,
Asali hii si tamu, mate yanakuchezea!

Yatakiwa ya maua, nyuki  kutochakachua,
Mizingani kulelewa, na kisha ikapepewa,
Kwa ufundi kutolewa, panna kitu kutiwa,
Asali hii si tamu, mate yanakuchezea!

Sukari inayotiwa, hauachi kuijua,
Guru ikiongezewa, rangiye utaijua,
Ya kweli isiyokuwa, wala dawa haitakuwa,
Asali hii si tamu, mate yanakuchezea!

Shamaba  nimelinuia, kwenda kujianzishia,
Mizinga nikaitia, na nyuki kuangalia,
Umri ukishaingia, ya kweli kujipatia,
Asali hii si tamu, mate yanakuchezea!



No comments: