Tuesday, December 11, 2012

Visa mia vya kulia

Ifurahie dunia, japo maudhi yajaa,
Ukilia mara mia, elfu utajichekea,
Kifua ni kukiachia, upate vyema pumua,
Visa mia vya kulia, na elfu ni kuchekea!

Visa mia vya kulia, katika hii dunia,
Ila kila ikitokea, elfu pia huzua,
Fursa kujichekea, au tabasamu kuwa,
Visa mia vya kulia, na elfu ni kuchekea!

Ukiikasirikia, haumii dunia,
Wewe ni kujiachia, swingi likaitikia,
Mradi ukatambua, nuumba yake kutoa,
Visa mia vya kulia, na elfu ni kuchekea!

Yakikuudhi kwa mia, elfu hufurahia,
Maisha kufurahia, dunia hupata dawa,
Watu ukisadia, tiba unaambulia,
Visa mia vya kulia, na elfu ni kuchekea!

Ucheshi ukiulea, dhiki utaziondoa,
Watu wakajinyanyua, miguu wasiokuwa,
Mikono wasiokuwa, nao wakakukumbatia,
Visa mia vya kulia, na elfu ni kuchekea!

Watu huwasisimua, wakaicheka dunia,
Kicheko wakiangua, ushindi wajipatia,
Hali kana watambua, bora juu linakaa,
Visa mia vya kulia, na elfu ni kuchekea!

Njia wameishaijua, hii ndio hupitia,
Kuumbwa kwa kuzaliwa, na ufu kutunukwa,
Siku wataingojea, kwa hamu kubwa ikawa,
Visa mia vya kulia, na elfu ni kuchekea!

Kufa wameshagundua, ni  njia kwenye dunia,
Ilo bora kufikia, dahari kwenda kukaa,
Nani wa kuwazuia, kutoicheka dunia,
Visa mia vya kulia, na elfu ni kuchekea!

No comments: