Monday, December 10, 2012

Vita iko vijijini


HAKIKA nimebaini, vita iko vijijini,
Yao maksha ni duni, yangoja yenu auni,
Wangalimo subirani, kuwa hivyo hadi lini ?
Mwapiga kambi mjini, vita iko vijijini!

Mmewatoa thamani, si watu sasa ni nyani,
Wanaishi viotani,  hizo si nyumba jamani,
Hawanayo afueni, warudipo mashambani,
Mwapiga kambi mjini, vita iko vijijini!

Wanasiasa amkeni, mhamie vijijini,
Kama kweli mwaamini, umma unayo thamani,
Basi umma vijijini, watosheke wa mjini,
Mwapiga kambi mjini, vita iko vijijini!

Kuna uongozi duni, watu wasioamini,
Wawa sasa mumiani, ardhi imo  sokoni,
Dhuluma za kihaini, zafanyika vijijini,
Mwapiga kambi mjini, vita iko vijijini!

Elimu huko ya chini, magazeti ya mjini,
Redio sijaamini, vijijiini sizioni,
Walia wa vijijini, betri zinawahini,
Mwapiga kambi mjini, vita iko vijijini!

Tivii hawazioni, umeme bado njiani,
Safariye si makini, kufika karne gani?
Wakubwa hawalioni, waishi kama zamani,
Mwapiga kambi mjini, vita iko vijijini!

Msiufanye utani, sasa wameshawachokeni,
Kuna siu mtabaini, ahadi zenu si shani,
Tena wasiwasikiezeni, muwatazame

mgongoni,
Mwapiga kambi mjini, vita iko vijijini!

Maji yao mtopeni, wanayatia kinywani,
Mitaro hawajabaini, sembese toka bombani ?
Umbali wake amini, hurudi hadi jioni,
Mwapiga kambi mjini, vita iko vijijini!

Kinamama taabani, bado wakasake kuni,
Nishati yaorehani, mazingira ni shakani,
Pangelikuwa mizani, kosa tungelibaini,
Mwapiga kambi mjini, vita iko vijijini!

Neema ivijijini, ila hatujaliamini,
Twalifanyia uhuni, sisi watoto wa mjini,
Tunawacheka shambani, wakiingia mjini,
Mwapiga kambi mjini, vita iko vijijini!

Za msingi ni auni, tuziandame hisani,
Maji wakishabaini, nusura kubwa nyumbani,
Na umeme kutohini, watafunguka vichwani,
Mwapiga kambi mjini, vita iko vijijini!

Tukaishi vijijini, wanasiasa mjini,
Kwa vitendo tusaini, tulikuwepo vitani,
Na mipango yumkini, kadhaa kuibaini,
Mwapiga kambi mjini, vita iko vijijini!

Ushirikiano amini, hakuna na vijijini,
Ila wetu na Japani, umetulia mezani,
Kisha nao Marekani, Dar wanaidhamini,
Mwapiga kambi mjini, vita iko vijijini!

Ushirika anzisheni, wa mjini na vijijini,
Masuala  mkabaini, kutatua kimizani,
Mazito kuwa mwanzoni, mepesi yawe

mwakani,
Mwapiga kambi mjini, vita iko vijijini!

No comments: