Saturday, December 29, 2012

Watu wagumu kulipa

NANI asiyewajua,  viumbe kwenye dunia,
Nini utawafanyia, hadhi wakairidhia,
Afrika, Tanzania, nani atakayekujua ?
Watu wagumu kulipa,  wa kunilipa ni Mola !

Maneno yahesabiwa, kitu cha bure yakawa,
Thamani wameyatoa, ovyo wajitapikia,
Haki hatukujaliwa, wengine kuangalia,
Watu wagumu kulipa,  wa kunilipa ni Mola !

Kila mtu yake njia, huko huko apitia,
Yako hawezi kujua, hata ukimwlezea,
Masikio huachia, maneno kujipitia,
Watu wagumu kulipa,  wa kunilipa ni Mola !

Ndiyo waliyojaliwa, vingine hawatakuwa,
Wepesi kutumikiwa, sio wa kutumikia,
Wataka kuheshimiwa, pasina ya kwangalia,
Watu wagumu kulipa,  wa kunilipa ni Mola !

Wataka kubarikiwa, pasina kubarikia,
Wanapenda kusifiwa, kwa wajibu kutimia,
Wanapenda kujengewa, si wewe kukujengea,
Watu wagumu kulipa,  wa kunilipa ni Mola !

Chini hukushindilia, juu wakijinyanyua,
Kilio ukikitoa, sufu mdomo hutia,
Kisha wakajisagia, mradi yao yakawa,
Watu wagumu kulipa,  wa kunilipa ni Mola !

Wepesi kujinyanyua, wagumu kukunyanyua,
Hupenda kushangiliwa, na wala si kuzomewa,
Ukubwa huukamia, wao upate wafaa,
Watu wagumu kulipa,  wa kunilipa ni Mola !

Wakaifanza hadaa, ufukara kuridhia,
Kisha ikawa sanaa, chumo la kujichumia,
Tahfifu hukataa, kisije kikapungua,
Watu wagumu kulipa,  wa kunilipa ni Mola !

Watu hawajajaliwa, kiongozi wa kufaa,
Nafasi wazichukua, yao ya kujijengea,
Ya wanacnhi kufulia, mtindo mmoja ukawa,
Watu wagumu kulipa,  wa kunilipa ni Mola !

No comments: