Monday, December 24, 2012

Dhambi zao

Zigo lawaelemea, wameishachanganyikiwa
Sasa wazungumzia, vya chooni vitambaa,
Wanataka kutumia, kujifutia mafua,
Dhambi zao zawatesa, nani kuwapa nusura ?

Waliitaka dunia, kwayo pupa na unaa,
Sasa yawatumbukia, na kuwatoa usaha,
Kila wakifikiria,  hawaoni pa kupitia,
Dhambi zao zawatesa, nani kuwapa nusura ?

Hali wanaishangaa, hadhi waliyowania,
Kisha wakafurahia, kwa mengi kujichumia,
Ndani wakalimbikia, hata yaliyo ukiwa,
Dhambi zao zawatesa, nani kuwapa nusura ?

Waikimbiza dunia, hadi mapafu yaiia,
Wataka kujikusanyia, matumboni kuvitia,
Pasina kuiachia, hewa ya kuitumia,
Dhambi zao zawatesa, nani kuwapa nusura ?

Hamu imewazidia, uchafu wajiachia,
Heshima yawakataa, wanatafuta ubaya,
Wahuni wakosa haya, majina kkuyachezea,
Dhambi zao zawatesa, nani kuwapa nusura ?

Busara wamefulia, ujinga waongelea,
Kale waliitangulia, visa vyao kuvizua,
Kila walilochimbua, takataka limekuwa,
Dhambi zao zawatesa, nani kuwapa nusura ?

Watu wanawanunua, si kwao kupalilia,
Ila kwenda kujinyea, kwenye mashamba ya jamaa,
Kila wanpoingia, walinzi wawazuia,
Dhambi zao zawatesa, nani kuwapa nusura ?

Hofu imewaingia, migongo wageuzia,
Kila wanapoingia, kwa kilio walakiwa,
Rangi wanazotumia, zaonekana hadaa,
Dhambi zao zawatesa, nani kuwapa nusura ?

Uchoyo wawaumbua, vijisenti wakitoa,
Wenyewe wajinunua, mifukoni kuhemua,
Afya inacheua, na siha inaungua,
Dhambi zao zawatesa, nani kuwapa nusura ?

Wanasambaza sanaa, hekaya nazo hadaa,
Watu wawachefua, chafya zawastua,
Vijani wavikimbia, nyoka wakvidhania,
Dhambi zao zawatesa, nani kuwapa nusura ?

Kiama wakidhania, hali liko mbali jua,
Jasho wanavyotoa, michirizi maji yawa,
Vindoo wavitumia, ja mvua kudakia,
Dhambi zao zawatesa, nani kuwapa nusura ?

Mizimu yawatokea, kuweweseka tabia,
Kilio wanaangua, usingizi wakatoa,
Kisha kitanda kukwea, nje mbio kutokea,
Dhambi zao zawatesa, nani kuwapa nusura ?

Utadhani malaria, kiwani imeingia,
Wanawafata jamaa, kaburini waishia,
Huko walikozikiwa, mhanga waliotoa,
Dhambi zao zawatesa, nani kuwapa nusura ?

Mali walichodhania, ufakiri wawatia,
Mahoka wawasumbua, hapana wa kutlia,
Walilolifikiria, si hilo lilotokea,
Dhambi zao zawatesa, nani kuwapa nusura ?

No comments: